Monday 10 June 2013

Wanafunzi Kidato cha Siota Ileje walilia walimu

Na Ibrahim Yasin, Ileje
WANAFUNZI wa kidato cha tano na sita wa Sekondari ya kutwa Ileje wamelalamikia kitendo cha walimu wao kushindwa kuingia darasani.

Akizungumza na Tanzania Daima, mmoja wa wanafunzi hao ambaye hakutaka kutajwa jina lake alisema kuwa walimu wamekuwa wavivu wa kuingia kwenye vipindi, ambapo tangu Januari hadi sasa (Juni) mwalimu mmoja ameingia darasani mara tatu.

Chanzo hicho kilisema kuwa walimu wa masomo ya kawaida hawafundishi huku wakidai kuwapo kwa uhaba wa walimu wa sayansi ambapo imekuwa vigumu kujifunza kulingana na hali halisi ya mazingira ya shule hiyo.Kwa upande wake Mkuu wa Shule hiyo, Gwakisa Mwakyeja, alikiri kuwapo kwa tatizo la walimu shuleni hapo na kudai kuwa atafuatilia kwa kina maendeleo ya shule hiyo.

Mwakyeja alisema kuwa tatizo lililopo katika shule hiyo ni kuwa na walimu wachache, hivyo wanajitahidi kufanya kila mbinu kuhakikisha wanafunzi hao wanapata vipindi kila siku.

“Tatizo la walimu kwa shule hii lipo pia kwa nchi nzima, hivyo ni tatizo la kitaifa, hivyo nimeshukuru hata kupewa hawa walimu japo ni wachache na nitazidi kukabiliana na changamoto hiyo kuhakikisha kuwa tunawapatia elimu ya kutosha,” alisema Mwakyeja.

Hata hivyo Ofisa Elimu Sekondari, Jimmy Nkwamu, alisema itabidi kuwa na upembuzi wa kindani ili kuweza kuwabaini walimu wanaotoroka darasani huku wakichukua mshahara kila mwisho wa mwezi.

Shule yenye miaka 42 haina vyoo


Mwalimu wa Shule ya Msingi ya Kibirashi iliyopo Wilaya ya Kilindi mkoani Tanga akionyesha choo cha muda kinachotumiwa na wanafunzi wa shule hiyo. Picha na Pamela Chilongola 

NILIJARIBU kuangaza huku na kule kutafuta choo kilipo ili nikajisaidie mara kushoto kwangu nakutana na kibanda kilichojengwa na nyasi huku  wanafunzi wakiwa wamepanga  foleni kuingia katika kibanda hicho.
Wakati nikijaribu kutafakari mbele yangu nakutana na mwalimu wa Shule ya Msingi ya Kibirashi iliyopo Wilaya ya Kilindi ambaye jina lake hakutaka kulitaja anasema, hicho ni choo cha wanafunzi ambacho wanajisaidia.
Ni miaka 42 imefika tangu Shule ya Msingi ya Kibarashi iliyopo wilayani Kilindi Mkoa wa Tanga kujengwa mwaka 1971 ikiwa haina vyoo vya kudumu hivyo uongozi wa shule wa wakati huo walilazimika kuchimba vyoo vya muda ili wanafunzi na walimu waweze kutumia.
Mkuu wa Shule ya Msingi hiyo, Fatuma Mahimbo anasema tokea mwaka 1971 shule hiyo ilipojengwa walimu na wanafunzi wanaendelea kutumia vyoo vya muda ambavyo ni hatari kwa usalama wa maisha yao.
Mahimbo anasema wanafunzi wapo zaidi ya 700 na walimu wa shule hiyo wanatumia vyoo vya muda vilivyochimbwa na uongozi wa shule hiyo.
Mahimbo anasema ameripoti shuleni hapo mwaka 2010 na kuikuta hali ya huduma ya vyoo ni mbaya, ambapo mwaka 2011 alijaribu kuomba fedha ya ujenzi wa vyoo hivyo kwenye Halmashauri ya Kilindi na kuelezwa kuwa mwaka huo wa fedha haijapangiwa kwenye bajeti.
““Mwaka 1971 shule hii ilijengwa bila ya kujengwa vyoo vya kudumu hivyo mimi hali hiyo nimeikuta nilikuja mwaka 2012 nimekikuta choo kilichopo hakifai kutumika hivyo tulilazimika kujenga choo cha nyasi kiweze kutumiwa na wanafunzi, huku walimu wakitumia choo kilichopo nyumbani kwangu ambayo ni nyumba ya walimu,”anasema Mahimbo.
Mahimbo anasema walikaa kikao cha kamati ya shule hiyo na kukubaliana suala hilo lipelekwe kwenye Serikali ya kijiji ili iweze kuwasaidia.
Anaeleza baada ya kuwasilisha suala hilo kwenye Serikali ya kijiji iliamua kujenga vyoo viwili kila kimoja kina matundu matano. Hivyo  ujenzi huo umeishia kwenye linta kutokana na Serikali ya kijiji hicho kuishiwa fedha.
“Ujenzi huu umesimama mwaka 2012 hivyo tumekaa kikao na wazazi na tumekubaliana kila mzazi atachangia Sh2000 kuanzia Julai mwaka huu”anasema Mahimbo.
Mahimbo anasema kutokana na hali hiyo aliyaomba mashirika na taasisi mbalimbali yajitokeze yaweze kusaidia ujenzi wa vyoo vya shule ili kuokoa afya za wanafunzi ambazo zipo hatarini na hata jamii inayowazunguka kupata magonjwa ya milipuko.
Anasema jamii haina mwamko wa elimu hawatambui suala la kuchangia ujenzi wa choo  linawahusu wao wanadhani suala hilo ni la mwalimu mkuu hivyo wanatakiwa kuchangia fedha ili ujenzi wa vyoo hivyo ukamilike.

Pia anasema kuna mchezo wa umeibuka kwa wazazi wenye watoto wa darasa la saba wanawashawishi watoto wao wasifanye bidii darasani ili wakae nyumbani kwa kukwepa gharama ya sekondari.

Tatizo hilo limekuwa sugu tumejaribu kukaa vikao vya mara kwa mara  na wazazi ili waweze kuwahimiza watoto wao wajisomee ili waweze kuwa kwenye nafasi nzuri ya kuchaguliwa kidato cha kwanza.

“Pia kuna Shirika la Kikristo la Misaada ya Binadamu (WVT) ambalo linasaidia kutoa elimu ili wazazi waachane na hii dhana potofu ya kumkataza mtoto asifahulu kwa kiasi kikubwa wazazi wameanza kubadilika,” alisema Mahimbo.

Wanafunzi wakianza  shule wanakuwa zaidi ya 70  wanapofika darasa la saba idadi inapungua na kufikia 25 hivyo wengi wao wanakuwa nyumbani kuwasaidia wazazi wao kazi za shamba na hata wengine wanaolewa wakiwa na umri mdogo sana.

Meneja Mradi wa Afya ya Mama na Mtoto wa Shirika la  Kikristo la Misaada ya Binadamu(WVT), Daudi Gumbo anasema wanatoa elimu katika jamii ili waweze kuwahamasisha watoto wao waende shuleni ili kuondokana na umaskini.

Gumbo anasema imekuwa ni kawaida kwa wazazi na walezi kujali uchangiaji wa harusi na sherehe nyinginezo huku wakisahau uchangiaji wa elimu hiyo.

“Kazi yetu tunatoa elimu katika  jamii ili kuwahamasisha jamii kuchangia elimu pale inapohitajika na tunatembelea shule mbalimbali kuangalia matatizo yaliyopo mfano Tarafa ya Mgela tumetoa vitabu mbalimbali, madawati na tumejenga madarasa ya shule,” alisema Gumbo.

Mkuu wa Wilaya hiyo Selemani Liwowa anasema tatizo la ukosefu wa vyoo hivyo bado halijawafikia  hivyo wanalifuatilia na kuthibitisha waweze kupata ufumbuzi.

Anasema mikakati ya wilaya hiyo ni kuondoa kero zinazozikabili shule mbalimbali ikikwemo madawati, ujenzi wa madarasa hivyo Shirika la WVT wamesaidia kwa kiasi kikubwa  kujenga vyumba vya madarasa kwenye shule mbalimbali.

 “Hilo tatizo hatujalipata rasmi hivyo tunalifuatilia na kuthibitisha ili tuweke mikakati ya jinsi gani ya kuondokana na tatizo hilo,”alisema Liwowa.
Chanzo:Mwananchi

SOMKI - FURSA YA UDHAMINI KWA AJILI YA WANAFUNZI WA KIKE WENYE VIPAJI LAKINI HAWAJIWEZI




Tunayo furaha kuwafahamisha kuwa kuna nafasi za udhamini kwa ajili ya wanafunzi wa kike wenye vipaji lakini wasiojiweza, chini ya Mradi wa Somesha Mtoto wa Kike (SOMKI). Mradi wa SOMKI unaleta utofauti katika maisha ya wanafunzi wa kike wa Tanzania wanaoishi katika mazingira magumu na wasiojiweza na ambao wameonyesha vipaji maalum au imeonekana kuwa na uwezo wa kufanya vizuri katika masomo yao na kufikia viwango vya juu au daraja la kwanza katika mitihani yao.

Udhamini huu ni kwa ajili ya kuhakikisha kwamba hawaathiriki na hali yao ya kimaisha ya sasa na kwamba wanaweza kupata fursa ya kubadilisha maisha na kuwa na maisha bora. Baada ya mchakato wa uhakiki na tathmini ya uhitaji itawapa walengwa fursa ya kupata elimu na kuwapunguzia mazingira magumu wanayoishi na kujisomea.

Tunaelewa kuwa katika shule yenu au utakuwa na taarifa kuwa kuna wanafunzi wanaostahili kupata nafasi hii. Kwa barua hii tunaomba uweze kusambaza taarifa hii na kuhamasisha wale wanaostahili kutuma maombi yao. Tafadhali nafasi hizi hutolewa mara moja tu kwa mwaka. Maombi haya yako wazi hadi kufikia tarehe 30 Desemba 2013, kwa ajili ya wanafunzi watakaodhaminiwa kitaaluma na Mradi wa SOMKI kwa mwaka 2014.

Maombi yatumwe kwenye anuani iliyopo hapo chini. Na kwa maelezo zaidi msisite kututafuta kwa anuani iliyopo hapo chini na namba ya simu.

Mlalakuwa,  Mikocheni,   Plot No: 36 B,   P.O. Box 71821, 
 Dar es Salaam, Tanzania 
Email: sophiamkana@yahoo.com Tel: +255-0656 647 280


Wenu mtiifu,

 Jane M


Mratibu wa Mradi 


Walimu Ukerewe kuandamana kisa madeni


CHAMA cha Walimu Tanzania (CWT) Wilaya ya Ukerewe, mkoani  Mwanza kinakusudia kuitisha maandamano ya amani ili kushinikiza  serikali kuwalipa watumishi wa halmashauri ya wilaya hiyo mshahara wa mwezi uliopita.

Shinikizo hilo la CWT linakuja baada ya watumishi 2,500 wa kada tofauti  wakiwemo walimu kutolipwa mshahara wao wa mwezi uliopita hadi kufikia jana.

Katibu wa CWT Wilaya ya Ukerewe,  John Kafimbi alisema kuwa wanachama wake ambao ni walimu na hata watumishi wa kada nyingine,  tayari wameishiwa uvumilivu na  wapo tayari kufanya maandamano ya amani ya kudai haki yao.

Mwenyekiti wa CWT wa wilaya hiyo, Pastory Kabelinde, alisema ni jambo la kusikitisha kuona serikali  inashindwa kutimiza wajibu wake,  hasa kwa kutowalipa mhahara wa  watumishi wa mwezi uliopita hadi sasa.

Alisema suala hilo mbali ya  kuwavunja moyo watumishi, pia   linakiuka haki za binadamu kwa vile  hivi sasa watumishi hao na familia  zao wanashindwa kupata mahitaji  muhimu kama vile chakula.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa  Halmashauri hiyo, Godlive Nnko  alikiri kuwepo kwa tatizo hilo na kuwaomba watumishi hao kuwavumilivu wakati suala hilo likishughulikiwa.

Alisema hakuna sababu ya kufanya maandamano hayo kwa kuwa tatizo lililokuwepo limekwisha, na kuongeza kuwa kuanzia mwanzo mwa wiki ijayo mshahara wao utalipwa.

BAVICHA kuendesha kongamano la Elimu

Katibu Mkuu wa BAVICHA
BARAZA la Vijana wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (BAVICHA) limeandaa kongamano la kujadili elimu na mustakabali wa taifa linalofanyika leo mjini Dodoma katika Ukumbi wa Kilimani.
Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa BAVICHA, Deo Munishi, kongamano hilo limelenga kuwapa nafasi wanafunzi wa shule za msingi, sekondari na vyuo vyote mkoani humo kujadili matatizo na namna serikali itakavyoweza kujinasua katika janga hilo.
Munishi alisema wameamua kuitisha kongamano hilo baada ya kubaini kuwa moja ya matatizo makubwa yanayowakabili vijana nchini kwa muda mrefu sasa, ni ukosefu wa elimu bora inayokidhi viwango.
“Tumebaini kuwa tuna elimu isiyowaandaa vijana kuwa wataalamu kutokana na mahitaji halisi ya jamii yetu…BAVICHA imeamua kufanya kongamano hili ili ufumbuzi wa tatizo hili uweze kupatikana,” alisema Munishi.
Aliongeza kuwa kongamano hilo litakalowashirikisha walimu na wahadhiri, litajikita katika kuchambua namna mfumo wa uendeshaji na usimamizi wa sekta ya elimu unavyosababisha kuporomoka kwa sekta hiyo nyeti, na kisha kujadili njia mbadala za kusaidia kuondokana na vikwazo hivyo.
Katibu Mkuu huyo alisema mara baada ya uchambuzi wa hoja zitakazoibuliwa wakati wa mjadala wa kongamano hilo, BAVICHA itawasilisha maoni yake kwa uongozi wa CHADEMA Taifa kama sehemu ya mchango wa vijana nchini katika kuboresha sera ya elimu.