Tuesday 18 March 2014

Airtel yakabidhi Sh Mil 5 Tuzo za Mwanamakuka 2014

Afisa Uhusiano wa Airtel, Jane Matinde (kushoto) akimkabidhi mfano wa hundi Mwenyekiti UWF na Mratibu wa Mradi wa Tuzo za Mwanamakuka Maryam Shamo wakati wa hafla ya Tuzo za Mwanamakuka 2014 ambapo Airtel Tanzania ni moja kati ya Wadhamini wa tuzo hizo ambazo Leila Mwambungu  aliibuka mshindi wa mwaka 2014. Wengine pichani kulia ni Mkurugenzi  Mkuu wa TWB Bi Margreth Chacha.
Afisa Uhusiano wa Airtel, Jane Matinde (kulia) akimpongeza mshindi wa tuzo ya Mwanamakuka 2014 Leila Mwambungu mara baada ya kutangazwa katika hafla iliyofanyika Escape One, Mikocheni Dar es Saalam.
Mshindi wa Tuzo za Mwanamakuka 2014, Leila Mwambungu akitoa shukrani zake mara baada ya kutangazwa katika hafla iliyofanyika Escape One siku ya Jumamosi. Kulia kwake ni Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Wanawake Tanzania (TWB) Margreth Chacha.
KAMPUNI ya simu za mkononi ya Airtel, imekabidhi waandaaji wa Tuzo za Mwanamakuka, Umoja wa Wanawake Marafiki (UWF) kiasi cha Sh. Mil. 5 wakati wa hafla ya utoaji wa tuzo za Mwanamakuka-2014 zilizofanyika jijini Dar es Saalam, ambapo Leila Mwambungu aliibuka mshindi wa mwaka huu akiwabwaga washiriki wenzake tisa aliochuana nao.
Tuzo ya mwaka huu ilishirikisha washindi 10, watano wa mwaka 2012 na wengine wa mwaka 2013 kupima mafanikio yao kibiashara baada ya kunyakua tuzo na zawadi ya fedha katika shindano hilo lililoasisiwa mwaka juzi.
Mshindi huyo aliyekuwa mshindi wa pili wa tuzo za mwaka jana, aliibuka kidedea baada ya barua iliyoeleza alipotokea, alipo na malengo yake baada ya kushinda tuzo hiyo kutia fora na kumpa ushindi mbele ya wenzake.
Kampuni ya Airtel, imekuwa ikidhamini tuzo hizo tangu zilipoanzishwa safari hii ilikabidhi kiasi hicho cha fedha kupitia kwa Afisa Uhusiano wake, Jane Matinde aliyeeleza furaha waliyonayo kudhamini tuzo hizo kwa miaka mitatu mfululizo.
Matinde alisema Airtel wanajisikia faraja kuona wamekuwa sehemu ya kuleta mabadiliko kwa wanawake kupitia tuzo hiyo na kuahidi kuendelea kushirikliana na UWF kuhakikisha mabadiliko hayo yanawafikia wanawake wengi zaidi nchini.
“Tutaendelea kushirikiana na UWF, ili kuhakikisha tunawafikia wanawake wengi zaidi nchini,” alisema Matinde.
Kwa upande wa mshindi wa Mwanamakuka 2014, Leila Mwambungu alisema amejisikia furaha sana kushinda tuzo hiyo akidai hakuwa ametegemea na kuwashukuru waandaaji na wadhamini wake na kuomba waendelee kuwasaidia kuwakwamua wanawake nchini ambao wamejitosa kwenye shughuli za ujasiriamali.
"Naona fahari na furaha kuwa mshindi wa tuzo hizi za mwanamakuka kwa mwaka huu, napenda kuwashukuru sana waandaaji wa tuzo hizi kwa kuniona kupitia juhudi ninazoziweka katika kazi zangu na biashara zangu. Mpaka sasa nimeweza kuajiri watanzania kupitia biashara zangu. Kiasi nilichozawadiwa kitanisaidia kukuza zaidi mtaji wangu. Nashukuru sana," alisema mshindi huyo.
Naye Mwenyekiti UWF na Mratibu wa Mradi wa Tuzo ya Mwanamakuka, Mariam Shamo alisema tuzo hiyo inaendelea kukua na kuzidi kuiboresha na kudai lengo la shindano la mwaka huu lilikuwa kupima maendeleo ya washindi wao 10 kuona jinsi gani biashara zao zinavyosonga mbele baada ya kumzawadia aliyefanya vizuri zaidi.
"Tunashukuru sana Airtel kwa kushirikiana nasi miaka mitatu kwa sasa na tunaamini kuwa bado wataendelea kutoa mchango wao na kushirikiana nasi na kutuunga mkono kwa miaka mengine ijayo na kuhakikisha lengo letu la kumwinua mwanamke wa kitanzania linafikiwa," alisema Mariam.
Washiriki wa tuzo za mwaka huu walikuwa ni Tatu Ngao, Mwananne Msekalile, Sikudhani Daudi na Nasra Aziz walioshinda mwaka 2012 na Aziza Mbogolume, Leila Mwambungu, Theonistina Renatus, Maajab Yusufu na Agnes Daudi walioshinda mwaka 2013.

Monday 17 March 2014

Wanawake msiwe tegemezi kwa kigezo cha kukosa ajira



Wanawake hawapaswi kuwa wanyonge
 WANAWAKE wametakiwa kutokuwa tegemezi kwa kigezo cha kukosa ajira, badala yake wajiunge katika vikundi  vya ujasiriamali ili kujenga misingi  bora ya familia zao.
Akizungumza jijini Dar es Salaam  juzi, Mratibu wa shirika lisilo la kiserikali Caritas linajihusisha na utoaji wa miradi  mbalimbali kwa kina mama, Glads Oning’o, alisema mwanamke ni nguzo ya familia, hivyo wajishughulishe ili kuzisaidia familia zao.
Alisema shirika hilo lina miradi ya kuwakopesha fedha kina mama  pamoja na mradi wa kilimo, ili waweze kujikomboa, kuondokana na hali tegemezi.

Huyu ndiye Mwanamakuka 2014

Hii ilikuwa mwaka jana niliponyakua ushindi wa pili
Wakati nakabidhiwa hundi ya ushindi wangu wa mwaka jana
Nikiwa na washindi wenzangu wa mwaka jana, Theonistina Renatus na Aziza Mbogolume
SIKU ya Jumamosi pale Escape One, kulifanyika Family Day iliyoambatana na utoaji wa Tuzo za Mwanamakuka 2014 inayoratibiwa na Umoja wa Wanawake Marafiki (UWF) chini ya udhamini wa Benki ya Wanawake Tanzania (TWB) na Airtel na wengineo.
Kwa tuzo zilifana mno, lakini kubwa ni kwamba mshindi wa Tuzo ya Mwanamakuka kwa 2014 hatimaye alipatikana baada ya washiriki 10 walioshiriki na kushinda tuzo za mwaka 2012 na 2013 kushindanishwa kuandika barua kuonyesha kufanikiwa kwake na kufikia malengo baada ya ushindi waliopata miaka hiyo.
Miongoni mwa washiriki nilikuwa mimi mwenyewe Leila Mwambungu, mshindi namba mbili wa mwaka jana ( 2013).
Bahati nzuri, Mungu alikuwa upande wangu baada ya kuibuka kidedea dhidi ya washiriki wenzangu.
Kwa hakika namshukuru Mungu kwa kuweza kunisaidia kushinda tuzo ya Mwanamakuka kwa mwaka 2014 na kama nilivyoandika katika barua yangu nitajitahidi kwa uwezo wa Allah (Subhanna Wataallah) kuwa mfano katika tuzo hizo na kuwasaidia wanawake wengine kuhamasisha kujikomboa kupitia ujasiriamali.
Tuzo hii ya Mwanamakuka ilianzishwa mwaka 2012 na Tatu Mwenda ndiye aliyeibuka kidedea mwaka huo wa kwanza akifuatiwa na Mwanne Msakalile.Mwaka jana mshindi wa kwanza alikuwa Aziza Mbogolume na kufuatiwa na mimi mwenyewe na nishukuru kwamba ushindi wa mwaka jana umeniwezesha kufikia malengo niliyokusudia, japo bado naendelea kupigana.
Ushindi wa mwaka huu ambao kwa hakika sikuutegemea kutokana na ushindani uliokuwapo kwa kujumuishwa washindi wote 10, watano wa mwaka 2012 na wengine wa mwaka jana.
Niwashukuru waratibu wa tuzo hiyo Umoja wa Wanawake Marafiki (UWF) na wadhamini wakuu Benki ya Wanawake Tanzania (TWB).
Pia shukrani zangu ziende kwa wote waliosaidia kwa namna moja wa nyingine kupata ushindi kwa miaka miwili mfululizo, hususani Mume Wangu ambaye amekuwa akinitia Moyo na kuwa bega kwa bega katika michakato hii na hata ninapovunjika moyo hunitia nguvu na kunisisitiza kuwa 'Wanawake Wanaweza na Katu Hawakati Tamaa'.
Kwa washiriki wenzangu wanashukuru pia na kuwataka tuendelee kushirikiana kuonyesha mfano kwa wengine na kujaribu kuwasaidia wanawake wengine nao wafikie malengo kama tulivyowezeshwa na UWF na TWB na hasa Bi. Mariam Shamo na Margareth Chacha.

Tusiruhusu ushoga nchini, hatari kwa taifa-Sheikh Muhenga



http://bloggerimports.files.wordpress.com/2008/12/img_2954-raisidd.jpg?w=640
Sheikh Mohammed Muhenga
SERIKALI imeombwa kufuata nyayo za serikali ya Uganda chini ya Rais Yoweri Museveni kwa kuktaa kuruhusu ushoga.
Serikali imeombwa kufuata nyayo za serikali ya Uganda chini ya Rais Yoweri Museveni kwa kukataa kuruhusu ushoga licha ya kuziudhi nchi za magharibi zinazokingia kifua vitendo hivyo.
Ombi hilo limetolewa na Imamu wa Msikiti wa Mwembechai, Sheikh Mohammed Muhenga, alipokuwa akiwahutubia waumini kabla ya swala ya Ijumaa iliyoswaliwa msikiti hapo, jijini Dar es Salaam.
Imamu Muhenga alisema kitendo cha Watanzania kunyamazia na kukumbatia matendo maovu yanayomchukiza Mungu vinaweza kuzua balaa kwa taifa.
"Tushirikiane kukemea maovu, tusinyamazie matendo yanayomchukiza Mungu kwani hakuna anayeweza kuhimili ghadhabu za Mungu akiamua kutuadhibu,"alisema .
Sheikh huyo alisema vitendo vya ulevi, biashara ya watu kujiuza, ujambazi na matendo mengine kwa kisingizio cha kukabiliana na hali ngumu ya maisha vinapaswa kuepukwa kwa nguvu zote.
"Huku ni sawa na kumbeep Mungu, je akiamua kutupigia tupo tayari kuhimili ghadhabu yake, tukemee maovu na kukemea kwani Mtume Muhammad (Sallallah Aley Wasalam) anasema miongoni mwa dalili 10 za kiama ni umma wake kugeuza pombe kuwa chai, watu kurejea enzi za Kaum Lut," alisema.
Sheikh alisema matendo vya ushoga na maovu mengine ni kuvuka mipaka kwa wanadamu ya uumbaji na humchukiza Mungu, hivyo ni wajibu wa kila mtu kukemea na kuyakataa matendo hayo.
Hivi karibuni Uganda ilipitisha sheria kali dhidi ya vitendo vya ushoga na kukera nchi ya Marekani na washirika kwake ambao wameruhusu vitendo hivyo katika nchi zao licha ya kwenda kinyume na mafundisho ya kidini.
Katika vitabu vya kuanzia Qur'an mpaka Biblia inasimulia kisa cha watu wa Nabii Lutu walivyotakabari na kuwaendea wanaume wenzao wakiwaacha wanawake na Mungu akawaadhibu adhabu inayoelezwa haijawahi kupewa wanadamu kama hiyo.