|
Waziri wa Elimu na Ufundi Stadi, Dk Shukuru Kawambwa |
MARA nyingi jamii imekuwa ikiinyoshea kidole serikali na kuwatupia lawama walimu na wasimamizi wa elimu nchini kutokana na matokeo mabaya ya mitihani ya kitaifa.
Hata sasa mijadala inayoendelea mtaani ni juu ya matokeo yaliyotangazwa hivi karibuni na Baraza la Taifa la Mitihani, NECTA,yanayohusu mitihani ya kidato cha nne na cha pili, ambayo yamekuwa na ufaulu mdogo kulinganisha na mwaka uliopita.
Kilichowachefua zaidi watu ni namna shule za serikali ambazo ni kilimbilio na tegemeo kwa wengi kwa miaka mingi, zimeanguka vibaya zikiachwa mbali na shule binafsi.
Yawezekana serikali inastahili lawama kwa kuwepo kwa matokeo hayo mabovu ya shule zake, pia kudidimia kwa kiwango cha elimu nchini kunakosababishwa na kushindwa kusimamia vema sekta hiyo kwa kuwatengenezea mazingira mazuri walimu.
Hakuna asiyejua kwa sasa nchini walimu wamekuwa ndio watumishi wa serikali dhalili kwa namna walivyosahauliwa wakicheleweshewa mishahara yao na malimbikizo ya pohso zao kiasi cha kuwavunja moyo wa kufundisha shuleni.
Leo walimu wamezigeuza shule wanazofundishia kuwa vijiwe vya kupiga soga na kuuza maandazi, ubuyu, kababu na karanga na kuwalazimisha wanafunzi kununua na kwenda na fedha za ziada shuleni kwa ajili ya masomo ya ziada.
Mtu unaweza kujiuliza mwalimu asiyeweza kumfundisha mtoto kwa muda wa kawaida wa masomo yaani saa 2 asubuhi hadi saa 8 mchana, anapataje muda wa kumsaidia mwanafunzi kwa masaa mawili ya masomo ya ziada?
Hata hivyo unabaini kuwa uwajibikaji mdogo na kukosa wito wa kazi ndio chanzo cha walimu wengi kuwa na 'mdadi' wa masomo ya ziada kwa vile unamuingizia pato nje ya pato lake halali la mshahara kama mtumishi wa serikali.
Hayo yote yanatokea siku hizi katika shule zetu kutokana na udhaifu ambao umekuwa ukionyeshwa na serikali na wasimamizi wa elimu katika kuhakikisha walimu wanalipwa fedha zao na kwa wakati pamoja na kupewa motisha mara kwa mara.
Licha ya kwamba uzembe huo unaofanywa na serikali katika usimamizi wa sekta ya elimu, bado jamii hususani wazazi na walezi nao wanapaswa kubeba mzigo wa lawama katika kuanguka kwa kiwango cha elimu nchini badala ya wenyewe kuwanyooshea wengine vidole.
Jamii kwa namna moja au nyingine ni sababu ya kuporomoka kwa kiwango cha elimu nchini kutokana na kutofuatilia kwa karibu maendeleo ya watoto wao wala kujua kama wanafika shuleni, wanasoma nini na wanafanya nini watokapo shuleni.
Nalisema hili nikirejea taarifa zilizotolewa na uongozi wa baraza la mitihani la taifa kwa mwaka wa pili mfululizo, baadhi ya watahiniwa na kidato cha nne kujibu maswali kwa kuandika na kuchora mambo machafu pamoja na kuandika nyimbo za Bongofleva.
Wanafunzi wanaofikia hatua ya kujibu au kuchora matusi kwenye karatasi za majibu ya mitihani yao, huenda hawana misingi mizuri ya malezi bora na wasiofuatiliwa na wazazi wao na hivyo kwenda shuelni sio kwa ajiliu ya kusoma bali kujifunza uhuni.
Kwa mwanafunzi mwenye kuachiwa hafanye atakalo bila kufuatiliwa na mzazi, hatma yake ni kwamba aingiapo kwenye mitihani huwa hana cha kujibu zaidi ya kuandika 'utumbo' kama huo wakiamini mradi wanamaliza mitihani yao na kupumzika.
Hapo ndipo mzazi anapolazikika kubeba mzigo wa lawama kwa matendo ya mtoto wa namna hiyo, naamini kama mzazi au mlezi ni mfuatiliaji wa maendeleo ya mwanae shuleni ni rahisi kugundua udhaifu wa mwanae na kumsaidia ikiwezekana 'kumnyoosha' kimaadili.
Lakini kwa vile wazazi wapo 'bize' kuhangaikia maisha na kusahau wajibu wao, ndio matokeo ya watoto hao kufanya madudu katika mitihani na matokoe yakitoka akiwa amefeli lawama zinaelekezwa kwa serikali na walimu wakati yeye mwenyewe ni chanzo.
Hivyo nilikuwa nawaasa wazazi na walezi, kuwa karibu na watoto wao na kufuatilia nyendo zao shuleni, kuwaacha watoto waishi kama kuku wa kienyeji bila kujua shuleni huenda kufanya nini, tutaendelea kushuka kwa kiwango cha elimu kila kukicha.
Ni kweli serikali wanapaswa kuboresha sekta ya elimu kadri iwezavyo, pia walimu kutekeleza wajibu wao ipasavyo, lakini wazazi na walezi hawapaswi kuwa watazamaji, wao wanapaswa kusimama kidete kuhakikisha mambo yananyooka kuanzia kwa watoto wao.
Kadhalika wanafunzi anapaswa kutambua wanapelekwa shuleni kujifunza na kusoma kwa faida yao, hivyo wakifuate kilichowapeleka na mambo ya kihuni na mengine ya kuiga ni kujiharibia mustakabali wa maisha yao ya baadae.
Kwa dunia ya sasa mtu bila elimu ni sawa na redio bila ya betri, waache kufanya ujinga na kuiga mambo ambayo hayana faida kwao hata kama wazazi na walezi wao hawafuatilii nyendo zao kwani mambo yanapoharibika hayawaharibikii wazazi au walezi wao bali wao wenyewe na siku zote majuto huwa mjukuu.