Tuesday, 2 April 2013

Mbunge Chalinze kuziwekea shule za jimbo lake umeme wa Jua


Mbunge wa Chalinze, Said Bwanamdogo aliyefadhili mradi wa umeme wa jua shuleni.
SHULE zilizopo katika Jimbo la Chalinze Wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani zinatarajiwa kunufaika na umeme wa jua.

Umeme huo utaunganishwa na wataalamu kwa ufadhili wa Mbunge wa jimbo hilo, Said Bwanamdogo.

Akizungumza hivi karibuni mjini hapa, Bwanamdogo alisema mkakati huo unatarajia kukamilika muda mfupi ujao baada ya wataalamu hao kukamilisha maandalizi ya awali.

Alisema lengo la kuunganisha umeme huo ni kuongeza ufanisi kwa wanafunzi na walimu katika sekta ya elimu.

Mbunge huyo alisema mbali na shule za jimbo hilo, pia nyumba za walimu zitaunganishwa umeme ili kuwavutia zaidi kufundisha katika shule za jimbo hilo.

“Lengo letu ni kuongeza ufaulu kwa wanafunzi katika jimbo letu, lakini pia kuweka mvuto kwa walimu wanapopangiwa katika shule zetu wasiombe uhamisho, waendelee kufundisha,” alisema.

Pamoja na hayo mbunge huyo aliwasihi wazazi kuwa na ushirikiano wa karibu na walimu wanaopangiwa kufundisha katika shule za maeneo yao, ili waweze kuongeza ufaulu kwa wanafunzi.

No comments:

Post a Comment