Picha hii haihusiani na habari hii, ila kwa idadi kubwa ya wanafunzi kama hii walimu watafundishaje? |
SHULE ya Msingi Sikonge, iliyopo mkoani Tabora kitengo cha elimu maalumu kwa walemavu, inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwamo ya ukosefu wa walimu.
Afisa Elimu Maalum wilayni Sikonge, Egata Magafu aliwaambia waandishi wa habari mkoani humo kuwa, shule hiyo iliyoanzishwa mwaka 2011 ina walimu watatu, wakati mahitaji halisi kulingana na idadi ya wanafunzi waliopo ni walimu nane.
“Shule kwa sasa ina wanafunzi 52, hivyo wanahitajika walimu nane na watumishi tisa, lakini kwa sasa wako
watatu tu hivyo kuwapa wakati mgumu wanafunzi kupata elimu bora,” alisema.
Mbali na hilo, alisema changamoto nyingine ni upungufu wa vyumba vya madarasa, vitendea kazi na wazazi kuwaficha watoto kutokana na imani potofu.
Alisema wanahitaji vyumba vya madarasa sita, ofisi za walimu mbili, nyumba za watumishi 14 na chumba
kwa ajili ya kufundishia watoto wenye ulemavu wa kutosikia.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Elimu Maalumu Wilaya ya Sikonge, Malaki Gumato, alisema
licha ya changamoto hizo, wamefanikiwa kujenga vyumba vya madarasa vinne na bweni moja.
Alisema mafanikio mengine ni kuongezeka kwa wanafunzi kutoka watano shule ilipoanzishwa hadi 52,
kujenga choo chenye matundu manne, kisima kimoja cha maji, tanki la kuvuna maji lenye uwezo wa ujazo
wa lita 5,000 na kufanikiwa kupata baadhi ya vifaa vya kufundishia kwa ajili ya walemavu wa macho.
Shule hiyo ilianzishwa kwa lengo la kutoa elimu kwa walemavu wa macho, albino, wenye uono hafifu na
viziwi.
No comments:
Post a Comment