Tuesday, 2 April 2013

Wanafunzi watoro kukiona Tabora



HALMASHAURI ya Wilaya ya Sikonge mkoani Tabora imesema inawasaka watoto 576 ambao hawajaripoti katika shule za sekondari.

Akizungmza na waandishi wa habari jana, Ofisa Elimu wa shule za sekondari Wilaya ya Sikonge Kiyungi Kasswa, alisema watoto hao walifaulu mitihani ya darasa la saba, lakini hadi sasa hawajaripoti shuleni.

Alisema wanafunzi walioripoti shule hadi sasa ni 846 kati ya 1,428 waliofanya mitihani ya kuhitimu darasa la saba mwaka jana.

Kasswa alisema kati watoto 567 ambao hawajaripoti shule, wa kiume ni 287 na wasichana 280.

Alisema wamejiwekea utaratibu ambao utasaidia kuwapata watoto hao na kuwarejesha shule sanjari na wazazi ama walezi wao kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria.

Alisema moja ya mikakati hiyo pia wameagiza viongozi wote kuanzia ngazi ya vitongoji, vijiji na kata kuhakikisha wanaanza kuwasaka watoto wote na wanaripoti shule haraka.

Kasswa aliongeza changamoto moja ambayo mara nyingi imekuwa chanzo cha watoto kukacha shule ni umbali mrefu, kwani watoto wanatembea kilomita zaidi ya 20 hadi 46 kufuata shule.

Hata hivyo, alisema wanajitahidi kuanza ujenzi wa hosteli, hali ambayo itasaidia kupunguza utoro ikiwemo kupikiwa chakula shuleni.





CHANZO:TANZANIA DAIMA

No comments:

Post a Comment