Monday 17 March 2014

Huyu ndiye Mwanamakuka 2014

Hii ilikuwa mwaka jana niliponyakua ushindi wa pili
Wakati nakabidhiwa hundi ya ushindi wangu wa mwaka jana
Nikiwa na washindi wenzangu wa mwaka jana, Theonistina Renatus na Aziza Mbogolume
SIKU ya Jumamosi pale Escape One, kulifanyika Family Day iliyoambatana na utoaji wa Tuzo za Mwanamakuka 2014 inayoratibiwa na Umoja wa Wanawake Marafiki (UWF) chini ya udhamini wa Benki ya Wanawake Tanzania (TWB) na Airtel na wengineo.
Kwa tuzo zilifana mno, lakini kubwa ni kwamba mshindi wa Tuzo ya Mwanamakuka kwa 2014 hatimaye alipatikana baada ya washiriki 10 walioshiriki na kushinda tuzo za mwaka 2012 na 2013 kushindanishwa kuandika barua kuonyesha kufanikiwa kwake na kufikia malengo baada ya ushindi waliopata miaka hiyo.
Miongoni mwa washiriki nilikuwa mimi mwenyewe Leila Mwambungu, mshindi namba mbili wa mwaka jana ( 2013).
Bahati nzuri, Mungu alikuwa upande wangu baada ya kuibuka kidedea dhidi ya washiriki wenzangu.
Kwa hakika namshukuru Mungu kwa kuweza kunisaidia kushinda tuzo ya Mwanamakuka kwa mwaka 2014 na kama nilivyoandika katika barua yangu nitajitahidi kwa uwezo wa Allah (Subhanna Wataallah) kuwa mfano katika tuzo hizo na kuwasaidia wanawake wengine kuhamasisha kujikomboa kupitia ujasiriamali.
Tuzo hii ya Mwanamakuka ilianzishwa mwaka 2012 na Tatu Mwenda ndiye aliyeibuka kidedea mwaka huo wa kwanza akifuatiwa na Mwanne Msakalile.Mwaka jana mshindi wa kwanza alikuwa Aziza Mbogolume na kufuatiwa na mimi mwenyewe na nishukuru kwamba ushindi wa mwaka jana umeniwezesha kufikia malengo niliyokusudia, japo bado naendelea kupigana.
Ushindi wa mwaka huu ambao kwa hakika sikuutegemea kutokana na ushindani uliokuwapo kwa kujumuishwa washindi wote 10, watano wa mwaka 2012 na wengine wa mwaka jana.
Niwashukuru waratibu wa tuzo hiyo Umoja wa Wanawake Marafiki (UWF) na wadhamini wakuu Benki ya Wanawake Tanzania (TWB).
Pia shukrani zangu ziende kwa wote waliosaidia kwa namna moja wa nyingine kupata ushindi kwa miaka miwili mfululizo, hususani Mume Wangu ambaye amekuwa akinitia Moyo na kuwa bega kwa bega katika michakato hii na hata ninapovunjika moyo hunitia nguvu na kunisisitiza kuwa 'Wanawake Wanaweza na Katu Hawakati Tamaa'.
Kwa washiriki wenzangu wanashukuru pia na kuwataka tuendelee kushirikiana kuonyesha mfano kwa wengine na kujaribu kuwasaidia wanawake wengine nao wafikie malengo kama tulivyowezeshwa na UWF na TWB na hasa Bi. Mariam Shamo na Margareth Chacha.

No comments:

Post a Comment