Afisa Uhusiano wa Airtel, Jane Matinde (kulia) akimpongeza mshindi wa tuzo ya Mwanamakuka 2014 Leila Mwambungu mara baada ya kutangazwa katika hafla iliyofanyika Escape One, Mikocheni Dar es Saalam. |
Tuzo ya mwaka huu ilishirikisha washindi 10, watano wa mwaka 2012 na wengine wa mwaka 2013 kupima mafanikio yao kibiashara baada ya kunyakua tuzo na zawadi ya fedha katika shindano hilo lililoasisiwa mwaka juzi.
Mshindi huyo aliyekuwa mshindi wa pili wa tuzo za mwaka jana, aliibuka kidedea baada ya barua iliyoeleza alipotokea, alipo na malengo yake baada ya kushinda tuzo hiyo kutia fora na kumpa ushindi mbele ya wenzake.
Kampuni ya Airtel, imekuwa ikidhamini tuzo hizo tangu zilipoanzishwa safari hii ilikabidhi kiasi hicho cha fedha kupitia kwa Afisa Uhusiano wake, Jane Matinde aliyeeleza furaha waliyonayo kudhamini tuzo hizo kwa miaka mitatu mfululizo.
Matinde alisema Airtel wanajisikia faraja kuona wamekuwa sehemu ya kuleta mabadiliko kwa wanawake kupitia tuzo hiyo na kuahidi kuendelea kushirikliana na UWF kuhakikisha mabadiliko hayo yanawafikia wanawake wengi zaidi nchini.
“Tutaendelea kushirikiana na UWF, ili kuhakikisha tunawafikia wanawake wengi zaidi nchini,” alisema Matinde.
Kwa upande wa mshindi wa Mwanamakuka 2014, Leila Mwambungu alisema amejisikia furaha sana kushinda tuzo hiyo akidai hakuwa ametegemea na kuwashukuru waandaaji na wadhamini wake na kuomba waendelee kuwasaidia kuwakwamua wanawake nchini ambao wamejitosa kwenye shughuli za ujasiriamali.
"Naona fahari na furaha kuwa mshindi wa tuzo hizi za mwanamakuka kwa mwaka huu, napenda kuwashukuru sana waandaaji wa tuzo hizi kwa kuniona kupitia juhudi ninazoziweka katika kazi zangu na biashara zangu. Mpaka sasa nimeweza kuajiri watanzania kupitia biashara zangu. Kiasi nilichozawadiwa kitanisaidia kukuza zaidi mtaji wangu. Nashukuru sana," alisema mshindi huyo.
Naye Mwenyekiti UWF na Mratibu wa Mradi wa Tuzo ya Mwanamakuka, Mariam Shamo alisema tuzo hiyo inaendelea kukua na kuzidi kuiboresha na kudai lengo la shindano la mwaka huu lilikuwa kupima maendeleo ya washindi wao 10 kuona jinsi gani biashara zao zinavyosonga mbele baada ya kumzawadia aliyefanya vizuri zaidi.
"Tunashukuru sana Airtel kwa kushirikiana nasi miaka mitatu kwa sasa na tunaamini kuwa bado wataendelea kutoa mchango wao na kushirikiana nasi na kutuunga mkono kwa miaka mengine ijayo na kuhakikisha lengo letu la kumwinua mwanamke wa kitanzania linafikiwa," alisema Mariam.
Washiriki wa tuzo za mwaka huu walikuwa ni Tatu Ngao, Mwananne Msekalile, Sikudhani Daudi na Nasra Aziz walioshinda mwaka 2012 na Aziza Mbogolume, Leila Mwambungu, Theonistina Renatus, Maajab Yusufu na Agnes Daudi walioshinda mwaka 2013.