Monday 10 June 2013

Shule yenye miaka 42 haina vyoo


Mwalimu wa Shule ya Msingi ya Kibirashi iliyopo Wilaya ya Kilindi mkoani Tanga akionyesha choo cha muda kinachotumiwa na wanafunzi wa shule hiyo. Picha na Pamela Chilongola 

NILIJARIBU kuangaza huku na kule kutafuta choo kilipo ili nikajisaidie mara kushoto kwangu nakutana na kibanda kilichojengwa na nyasi huku  wanafunzi wakiwa wamepanga  foleni kuingia katika kibanda hicho.
Wakati nikijaribu kutafakari mbele yangu nakutana na mwalimu wa Shule ya Msingi ya Kibirashi iliyopo Wilaya ya Kilindi ambaye jina lake hakutaka kulitaja anasema, hicho ni choo cha wanafunzi ambacho wanajisaidia.
Ni miaka 42 imefika tangu Shule ya Msingi ya Kibarashi iliyopo wilayani Kilindi Mkoa wa Tanga kujengwa mwaka 1971 ikiwa haina vyoo vya kudumu hivyo uongozi wa shule wa wakati huo walilazimika kuchimba vyoo vya muda ili wanafunzi na walimu waweze kutumia.
Mkuu wa Shule ya Msingi hiyo, Fatuma Mahimbo anasema tokea mwaka 1971 shule hiyo ilipojengwa walimu na wanafunzi wanaendelea kutumia vyoo vya muda ambavyo ni hatari kwa usalama wa maisha yao.
Mahimbo anasema wanafunzi wapo zaidi ya 700 na walimu wa shule hiyo wanatumia vyoo vya muda vilivyochimbwa na uongozi wa shule hiyo.
Mahimbo anasema ameripoti shuleni hapo mwaka 2010 na kuikuta hali ya huduma ya vyoo ni mbaya, ambapo mwaka 2011 alijaribu kuomba fedha ya ujenzi wa vyoo hivyo kwenye Halmashauri ya Kilindi na kuelezwa kuwa mwaka huo wa fedha haijapangiwa kwenye bajeti.
““Mwaka 1971 shule hii ilijengwa bila ya kujengwa vyoo vya kudumu hivyo mimi hali hiyo nimeikuta nilikuja mwaka 2012 nimekikuta choo kilichopo hakifai kutumika hivyo tulilazimika kujenga choo cha nyasi kiweze kutumiwa na wanafunzi, huku walimu wakitumia choo kilichopo nyumbani kwangu ambayo ni nyumba ya walimu,”anasema Mahimbo.
Mahimbo anasema walikaa kikao cha kamati ya shule hiyo na kukubaliana suala hilo lipelekwe kwenye Serikali ya kijiji ili iweze kuwasaidia.
Anaeleza baada ya kuwasilisha suala hilo kwenye Serikali ya kijiji iliamua kujenga vyoo viwili kila kimoja kina matundu matano. Hivyo  ujenzi huo umeishia kwenye linta kutokana na Serikali ya kijiji hicho kuishiwa fedha.
“Ujenzi huu umesimama mwaka 2012 hivyo tumekaa kikao na wazazi na tumekubaliana kila mzazi atachangia Sh2000 kuanzia Julai mwaka huu”anasema Mahimbo.
Mahimbo anasema kutokana na hali hiyo aliyaomba mashirika na taasisi mbalimbali yajitokeze yaweze kusaidia ujenzi wa vyoo vya shule ili kuokoa afya za wanafunzi ambazo zipo hatarini na hata jamii inayowazunguka kupata magonjwa ya milipuko.
Anasema jamii haina mwamko wa elimu hawatambui suala la kuchangia ujenzi wa choo  linawahusu wao wanadhani suala hilo ni la mwalimu mkuu hivyo wanatakiwa kuchangia fedha ili ujenzi wa vyoo hivyo ukamilike.

Pia anasema kuna mchezo wa umeibuka kwa wazazi wenye watoto wa darasa la saba wanawashawishi watoto wao wasifanye bidii darasani ili wakae nyumbani kwa kukwepa gharama ya sekondari.

Tatizo hilo limekuwa sugu tumejaribu kukaa vikao vya mara kwa mara  na wazazi ili waweze kuwahimiza watoto wao wajisomee ili waweze kuwa kwenye nafasi nzuri ya kuchaguliwa kidato cha kwanza.

“Pia kuna Shirika la Kikristo la Misaada ya Binadamu (WVT) ambalo linasaidia kutoa elimu ili wazazi waachane na hii dhana potofu ya kumkataza mtoto asifahulu kwa kiasi kikubwa wazazi wameanza kubadilika,” alisema Mahimbo.

Wanafunzi wakianza  shule wanakuwa zaidi ya 70  wanapofika darasa la saba idadi inapungua na kufikia 25 hivyo wengi wao wanakuwa nyumbani kuwasaidia wazazi wao kazi za shamba na hata wengine wanaolewa wakiwa na umri mdogo sana.

Meneja Mradi wa Afya ya Mama na Mtoto wa Shirika la  Kikristo la Misaada ya Binadamu(WVT), Daudi Gumbo anasema wanatoa elimu katika jamii ili waweze kuwahamasisha watoto wao waende shuleni ili kuondokana na umaskini.

Gumbo anasema imekuwa ni kawaida kwa wazazi na walezi kujali uchangiaji wa harusi na sherehe nyinginezo huku wakisahau uchangiaji wa elimu hiyo.

“Kazi yetu tunatoa elimu katika  jamii ili kuwahamasisha jamii kuchangia elimu pale inapohitajika na tunatembelea shule mbalimbali kuangalia matatizo yaliyopo mfano Tarafa ya Mgela tumetoa vitabu mbalimbali, madawati na tumejenga madarasa ya shule,” alisema Gumbo.

Mkuu wa Wilaya hiyo Selemani Liwowa anasema tatizo la ukosefu wa vyoo hivyo bado halijawafikia  hivyo wanalifuatilia na kuthibitisha waweze kupata ufumbuzi.

Anasema mikakati ya wilaya hiyo ni kuondoa kero zinazozikabili shule mbalimbali ikikwemo madawati, ujenzi wa madarasa hivyo Shirika la WVT wamesaidia kwa kiasi kikubwa  kujenga vyumba vya madarasa kwenye shule mbalimbali.

 “Hilo tatizo hatujalipata rasmi hivyo tunalifuatilia na kuthibitisha ili tuweke mikakati ya jinsi gani ya kuondokana na tatizo hilo,”alisema Liwowa.
Chanzo:Mwananchi

No comments:

Post a Comment