Monday, 10 June 2013

Walimu Ukerewe kuandamana kisa madeni


CHAMA cha Walimu Tanzania (CWT) Wilaya ya Ukerewe, mkoani  Mwanza kinakusudia kuitisha maandamano ya amani ili kushinikiza  serikali kuwalipa watumishi wa halmashauri ya wilaya hiyo mshahara wa mwezi uliopita.

Shinikizo hilo la CWT linakuja baada ya watumishi 2,500 wa kada tofauti  wakiwemo walimu kutolipwa mshahara wao wa mwezi uliopita hadi kufikia jana.

Katibu wa CWT Wilaya ya Ukerewe,  John Kafimbi alisema kuwa wanachama wake ambao ni walimu na hata watumishi wa kada nyingine,  tayari wameishiwa uvumilivu na  wapo tayari kufanya maandamano ya amani ya kudai haki yao.

Mwenyekiti wa CWT wa wilaya hiyo, Pastory Kabelinde, alisema ni jambo la kusikitisha kuona serikali  inashindwa kutimiza wajibu wake,  hasa kwa kutowalipa mhahara wa  watumishi wa mwezi uliopita hadi sasa.

Alisema suala hilo mbali ya  kuwavunja moyo watumishi, pia   linakiuka haki za binadamu kwa vile  hivi sasa watumishi hao na familia  zao wanashindwa kupata mahitaji  muhimu kama vile chakula.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa  Halmashauri hiyo, Godlive Nnko  alikiri kuwepo kwa tatizo hilo na kuwaomba watumishi hao kuwavumilivu wakati suala hilo likishughulikiwa.

Alisema hakuna sababu ya kufanya maandamano hayo kwa kuwa tatizo lililokuwepo limekwisha, na kuongeza kuwa kuanzia mwanzo mwa wiki ijayo mshahara wao utalipwa.

No comments:

Post a Comment