Monday 10 June 2013

Wanafunzi Kidato cha Siota Ileje walilia walimu

Na Ibrahim Yasin, Ileje
WANAFUNZI wa kidato cha tano na sita wa Sekondari ya kutwa Ileje wamelalamikia kitendo cha walimu wao kushindwa kuingia darasani.

Akizungumza na Tanzania Daima, mmoja wa wanafunzi hao ambaye hakutaka kutajwa jina lake alisema kuwa walimu wamekuwa wavivu wa kuingia kwenye vipindi, ambapo tangu Januari hadi sasa (Juni) mwalimu mmoja ameingia darasani mara tatu.

Chanzo hicho kilisema kuwa walimu wa masomo ya kawaida hawafundishi huku wakidai kuwapo kwa uhaba wa walimu wa sayansi ambapo imekuwa vigumu kujifunza kulingana na hali halisi ya mazingira ya shule hiyo.Kwa upande wake Mkuu wa Shule hiyo, Gwakisa Mwakyeja, alikiri kuwapo kwa tatizo la walimu shuleni hapo na kudai kuwa atafuatilia kwa kina maendeleo ya shule hiyo.

Mwakyeja alisema kuwa tatizo lililopo katika shule hiyo ni kuwa na walimu wachache, hivyo wanajitahidi kufanya kila mbinu kuhakikisha wanafunzi hao wanapata vipindi kila siku.

“Tatizo la walimu kwa shule hii lipo pia kwa nchi nzima, hivyo ni tatizo la kitaifa, hivyo nimeshukuru hata kupewa hawa walimu japo ni wachache na nitazidi kukabiliana na changamoto hiyo kuhakikisha kuwa tunawapatia elimu ya kutosha,” alisema Mwakyeja.

Hata hivyo Ofisa Elimu Sekondari, Jimmy Nkwamu, alisema itabidi kuwa na upembuzi wa kindani ili kuweza kuwabaini walimu wanaotoroka darasani huku wakichukua mshahara kila mwisho wa mwezi.

No comments:

Post a Comment