Monday 10 June 2013

BAVICHA kuendesha kongamano la Elimu

Katibu Mkuu wa BAVICHA
BARAZA la Vijana wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (BAVICHA) limeandaa kongamano la kujadili elimu na mustakabali wa taifa linalofanyika leo mjini Dodoma katika Ukumbi wa Kilimani.
Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa BAVICHA, Deo Munishi, kongamano hilo limelenga kuwapa nafasi wanafunzi wa shule za msingi, sekondari na vyuo vyote mkoani humo kujadili matatizo na namna serikali itakavyoweza kujinasua katika janga hilo.
Munishi alisema wameamua kuitisha kongamano hilo baada ya kubaini kuwa moja ya matatizo makubwa yanayowakabili vijana nchini kwa muda mrefu sasa, ni ukosefu wa elimu bora inayokidhi viwango.
“Tumebaini kuwa tuna elimu isiyowaandaa vijana kuwa wataalamu kutokana na mahitaji halisi ya jamii yetu…BAVICHA imeamua kufanya kongamano hili ili ufumbuzi wa tatizo hili uweze kupatikana,” alisema Munishi.
Aliongeza kuwa kongamano hilo litakalowashirikisha walimu na wahadhiri, litajikita katika kuchambua namna mfumo wa uendeshaji na usimamizi wa sekta ya elimu unavyosababisha kuporomoka kwa sekta hiyo nyeti, na kisha kujadili njia mbadala za kusaidia kuondokana na vikwazo hivyo.
Katibu Mkuu huyo alisema mara baada ya uchambuzi wa hoja zitakazoibuliwa wakati wa mjadala wa kongamano hilo, BAVICHA itawasilisha maoni yake kwa uongozi wa CHADEMA Taifa kama sehemu ya mchango wa vijana nchini katika kuboresha sera ya elimu.


No comments:

Post a Comment