Friday 17 May 2013

Dk Hosea aichangia Shule ya Sekondari Sh Mil. 10

http://3.bp.blogspot.com/-_zulXoZDlto/UGp3VbIUgQI/AAAAAAAAJCw/IhvsYRq0XCE/s1600/6.jpeg
Dk Hosea


MKURUGENZI Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini Dk. Edward Hosea ametoa sh milioni 10 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya maabara katika shule ya sekondari ya Binza iliyoko wilayani Maswa, Simiyu.

Akikabidhi fedha hizo jana kwa niaba yake Katibu Tawala wa wilaya ya Maswa, Danford Peter, mbele ya wanafunzi na walimu wa shule hiyo katika sherehe iliyofanyika shuleni hapo alisema hiyo ni utekelezaji wa ahadi aliyoitoa mwaka jana alipokutana na wazee wa mji huo.

Alisema kuwa Desemba 25 mwaka jana Dk. Hosea alikutana na baadhi ya wazee wa Nyalikungu yalipo makao makuu ya wilaya hiyo na mambo mengine walimwomba kusaidia ununuzi wa vifaa vya maabara katika shule hiyo.

“Dk. Hosea alipofika hapa kwa ajili ya mapumziko ya sikukuu ya Krismasi mwaka jana alionana na wazee wa mji huu na mazungumzo mengine walimwomba kusaidia ununuzi wa vifaa vya maabara na leo ametimiza ahadi yake na tunakabidhi hundi ya sh milioni 10 kwa uongozi wa shule ya Binza,” alisema.

Alisema kuwa kupatikana kwa vifaa hivyo kutawasaidia wanafunzi hao kujifunza kwa vitendo masomo ya sayansi ambayo mara nyingi hawayapendi kutokana na kutokuwepo kwa vifaa vya maabara.

Naye mkuu wa TAKUKURU wilayani hapa Daniel Ntera aliutaka uongozi wa shule hiyo kuzitumia fedha hizo kama ilivyokusudiwa na kwamba ofisi hiyo itafuatilia.

Akipokea hundi hiyo, mkuu wa shule ya Binza, Focus Nshiyiki, alimshukuru Dk. Hosea na kuahidi kuzitumia fedha hizo kama ilivyokusudia kwa kufuata kanuni, taratibu na sheria za manunuzi ya umma.

No comments:

Post a Comment