Rais wa CWT, Gratian Mukoba |
Onyo hilo lilitolewa jana na Mwenyekiti wa TTN, Faray Alfred, alipozungumza na waandishi wa habari jijini Mwanza kuhusiana na ukiukwaji wa sheria unaofanywa na CWT dhidi ya mwalimu.
Alfred alisema tangu CWT isajiliwe kisheria miaka ya 1992, imekuwa ikikiuka baadhi ya sheria za mfanyakazi wa taaluma ya ualimu, hivyo kusababisha walimu wengi kutonufaika na kazi ya chama hicho cha walimu.
Alisema tangu kuanzishwa kwake hadi sasa, CWT haiweki wazi mapato na matumizi kwa wanachama wake, ikiwa ni pamoja na kutokuwa na takwimu halisi za walimu ambao ni wanachama hai na mawakala wa ada, jambo linalotilia shaka uendeshwaji wa chama hicho.
“Uchunguzi uliofanywa na TTN umebaini CWT inakiuka sheria nyingi za nchi na Katiba ya Jamhuri ya Muungano. Kwanza inamkata mwalimu ada ya asilimia mbili pale anapoajiriwa bila ridhaa yake.
“Pili, CWT hawana mfumo wa kueleza mapato na matumizi, wala hawawaelezi wanachama wao kuhusu matumizi. Hili ni tatizo lazima timu ya TTN ambayo imesajiliwa kisheria mwaka jana itoe onyo kwa CWT,” alisema Alfred.
Kwa upande wake, mratibu wa TTN, Tungaraza Njugu alisema kwamba utendaji mbovu wa CWT ndiyo unaosababisha taaluma ya ualimu kushuka, kwani walimu wenyewe wameanza kukata tamaa.
“TTN tumesajiliwa kwa ajili ya kulinda na kutetea haki sheria za walimu. Kwa sasa tunafanya kampeni ya kuwaelimisha walimu jinsi CWT inavyowatendea ndivyo sivyo,” alisema.
Chanzo:Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment