Wednesday 8 May 2013

Mvua yasababisha upungufu wa madawati

   
WANAFUNZI 193 wanaosoma Shule ya Msingi Madaraka, Kata ya Mkwatani, wilayani Kilosa, Morogoro wanakaa chini kutokana na upungufu wa madawati.

Mwalimu Mkuu Msaidizi wa shule hiyo, Julieth Kalumwa, alisema jana kuwa wanafunzi wanaosoma darasa la awali na la kwanza wote wanakaa chini, na kwamba hiyo imechangiwa na madawati kuharibiwa vibaya na maji ya mafuriko.

Aliongeza kuwa wanafunzi wa darasa la pili na la saba pekee wanakaa kwenye madawati na kwamba madarasa yaliyosalia yana upungufu wa madawati na baadhi ya wanafunzi wanakaa chini.

Aidha, alisema shule hiyo kabla ya kukumbwa na mafuriko ilikuwa haina upungufu wa madawati, na kwamba yaliyokuwepo yalinyonya maji na hivyo kuharibika.

Mbali na hilo, alisema wanakabiliwa na uhaba wa vitabu vya kujifunzia na kufundishia, ambapo vya awali viliharibiwa na mafuriko, hivyo kupata wakati mgumu katika ufundishaji.

Kaimu Ofisa Elimu ya Msingi Wilaya ya Kilosa, Theodulis Mangia, alipoulizwa juu ya uhaba wa madawati alisema hilo ni la tatizo la wilaya nzima, huku akisema wanasubiri mgawo kutoka Tamisemi, ili kupunguza tatizo hilo.

No comments:

Post a Comment