Tuesday, 7 May 2013

Wanafunzi wageuka 'manamba' kusaka ada


WANAFUNZI wa kidato cha nne katika Shule ya Sekondari Mwangaza, iliyopo wilayani Mpanda, wako hatarini kufanya vibaya mitihani yao ya taifa kutokana na kutumia muda wa masomo kufanya vibarua ili waweze kupata fedha za kulipia ada na michango mbalimbali.

Mkuu wa shule hiyo, Simoni Lubange alibainisha hayo  mbele ya waandishi wa habari ambao walitembelea shuleni hapo hivi karibuni.

Alisema tatizo hilo lilianza mwaka jana baada shirika lisilo la kisekali la Shdepha Network lililokuwa likiwagharamia kuwasomesha kusitisha msaada huo.

Lubange alisema hali hiyo inaweza kuwafanya wanafunzi hao kufanya vibaya mtihani wao wa kumaliza kidato cha nne kutokana na kutumia muda wa masomo kufanya vibarua.

Mmoja wa wanafunzi hao, Sudi Mwimbula alisema kitendo cha shirika hilo kuacha kuwagharamia kumewaathiri kimasomo, kwani ndio waliokuwa wakiwapatia huduma zote shuleni.

Alisema si kama wanapenda kufanya vibarua mitaani, bali wanalazimika ili waweze kupata fedha za kulipia ada.

Mratibu wa Shdepha Network Wilaya ya Mpanda, EuzebiusNgurusha alisema shirika hilo lilikuwa likiwasomesha wanafunzi 312 kwa kuwalipia ada, sare za shule na vifaa mbalimbali vya matumizi ya shule.

Hata hivyo, alisema walilazimika kusitisha misaada hiyo baada ya wafadhili wao waliokuwa wakitoa misaada kwao kuisitisha mwaka jana, hali iliyolilazimu shirika hilo kuziandikia barua shule zote walizokuwa wakiwahudumia wanafunzi hao kuacha ufadhili.

No comments:

Post a Comment