Wednesday, 8 May 2013

Wanafunzi Umbwe wagoma kula

   
MGOGORO umeibuka katika Shule ya Sekondari Umbwe kati ya wanafunzi wa kidato cha tano na uongozi wa shule hiyo hali iliyosababisha baadhi ya wanafunzi kugoma kula na kufanya maandamano wakishinikiza kuonana na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro kwa lengo la kutatua kero zilizoko shuleni hapo.

Kutokana na mgogoro huo, Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Dk. Ibrahim Msengi aliyefika shuleni hapo kuutatua, alimtaka Ofisa Elimu Mkoa Kilimanjaro kupeleka wakaguzi katika shule mbalimbali za sekondari ikiwemo ya Umbwe ikiwa ni hatua mojawapo ya kubaini walimu wanavyotekeleza wajibu wao.

Akizungumza na uongozi wa shule hiyo pamoja na wanafunzi hao, Msengi alisema hatua ya ukaguzi katika shule za sekondari hasa za serikali, itabainisha uchafu uliojificha ambao unachangia kutofanya vizuri kwa shule hizo.

Dk. Msengi alisema licha ya madai ya wanafunzi hao kukiuka taratibu za kufikisha madai yao, bado yana msingi kutokana na ukweli kwamba wanalalamikia kutofundishwa baadhi ya masomo, jambo ambalo alieleza ndiyo chanzo cha kufeli kwa wanafunzi.

“Mengi ya madai haya yangeweza kutatuliwa hapa shuleni tena bila hata kumuita mtu yeyote,” alisema Msengi huku akiwaomba wanafunzi kuwa na subira wakati suala hilo likipatiwa ufumbuzi.

Dk. Msengi aliwataka wanafunzi kurudi darasani kuendelea na vipindi kama kawaida wakati wakisubiri utatuzi wa malalamiko yao.

Katika hatua nyingine mkuu huyo wa wilaya alimtaka mkuu wa shule hiyo, Silvanus Lyome kufuatilia kwa karibu utendaji kazi wa walimu wanaolalamikiwa kuhakikisha lugha zisizoeleweka hazitumiki katika malezi ya wanafunzi hao.

Chanzo:Tanzania Daima

No comments:

Post a Comment