Mbunge Joshua Nassari akiwa na baadhi ya wabunge wenzake wa Chadema |
WAFUGAJI Kimasai wametakiwa kuuza mifugo na kusomesha watoto wao ili wapate elimu itakayowawezesha kupata fursa mbalimbali za kiuchumi, kijamii na kisiasa kama jamii nyingine nchini.
Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari, alitoa wito huo katika harambee ya ujenzi wa shule ya sekondari katika eneo la Ngarbobo, wilayani Arumeru.
Nassari alisema jamii hiyo iko nyuma katika nyanja za kimaendeleo kutokana na kuendelea na mfumo wa ufugaji wa kuhamahama, jambo ambalo limesababaisha watoto wengi katika jamii hiyo kukosa fursa ya kupata elimu.
“Nawasihi ndugu zangu Wamasai sasa muanze kuwekeza katika elimu kwa watoto wenu nyakati hizi hakuna njia nyingine ya kutatua changamoto ni elimu pekee ndiyo njia ya kuweza kuleta faida isiyokwisha katika maisha yenu,” alisema Nassari.
Aidha mbunge huyo aliwapongeza wananchi wa eneo hilo kwa kujitokeza kwa wingi na kutoa mifugo kwa ajili ya ujenzi wa shule hiyo na kusema kuwa huo ndio mwanzo mpya wa jamii hiyo kuanza kubadilika kwa dhati na kuthamini elimu.
Aliwaambia wafugaji hao kwamba jamii hiyo imekuwa ikitoa viongozi waadilifu na wachapa kazi akiwemo waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowasa.
“Kwa asili mmejaliwa kuwa na watu wenye misimamo na maamuzi yenye masilahi kwa umma, wasomesheni watoto wenu ili waweze kutoa mchango katika kujenga taifa letu katika nyanja za kiuchumi na hata kisiasa,” alisema Nassari.
Aliwaambia wafugaji hao kuwa yeye alisoma katika hali ngumu na wakati fulani akisoma shule ya sekondari wazazi wake walilazimika kuuza kabati la vyombo, ili apate ada.
Alisema aliweza kusoma vizuri na kumaliza Chuo Kikuu ambapo sasa ana uwezo wa kununua kila anachokihitaji katika maisha yake na jamii yake.
Katika harambee hiyo wananchi walitoa ng’ombe zaidi ya 50 wenye thamani ya sh milioni 15, mbuzi na kondoo wenye tahamni ya sh milioni saba.
Harambee hiyo iliyoendeshwa na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Mkoa wa Arusha, Onesmo Nangole, kwa niaba ya Lowasa jumla ya sh milioni 53 zilipatikana
No comments:
Post a Comment