Thursday 9 May 2013

Wananchi Lindi wajitolea kumjengea nyumba mwalimu

Wakati mwingine vikao kama hivyo kati ya viongozi na wananchi husaidia kuamsha ari ya maendeleo ya maeneo husika.

WANANCHI wa kata ya Chiola Halmashauri ya Wilaya ya Nachingwea mkoani Lindi wamechanga kiasi cha Sh. Mil. 18.9 kwa ajili ya ujenzi wa nyymba wa Shule yao ya Sekondari ya kutwa.
Ofisa Mtendaji wa Kata hiyo, Patricia Mbunda alisema mradi huo wa nyumba hiyo ya mwalimu uliibuliwa na Kamati ya Maendeleo ya Kata yao pamoja na wananchi wa eneo hilo kwa nia ya kumuondolea kero mwalimu huyo na walimu wengine ambao pia wanatarajiwa kujengewa hapo baadaye.
Mbunda alisema mradi wao umekusudia kujenga nyumba saba za walimu ili kuwatatulia kero walimu wa shule hiyo na wazo hilo lilipowasilishwa kwa wananchi, wakazi hao walionyesha ushirikiano kwa kuchangia Sh  Mil.5.9 wakati serikali kuu imetoa Sh Mil 13.
Alisema mradi huo wa kuwajengea nyumba walimu wa shule ya kata yao ulianza rasmi katikati ya mwaka jana na anashukuru namna wakazi wa kata hiyo walivyoonyesha kujali na kuthamini maendeleo ya elimu katika eneo lao na kuwapongeza waendelee na moyo huo huo kwa manufaa ya kata yao na taifa kwa ujumla.
"Kwa sasa tuna nyumba moja tu ya walimu kati ya saba tulizopanga kuzijenga, ila tunashukuru wananchi walivyojitolea, japo kazi bado kabisa kwani walimu wengine sita wanaishi nyumba za kupanga ambazo hazina ubora unaendana na hadhi ya walimu," alisema.
Unadhani wananchi wa maeneo mengine wangeiga mfano huu wa Kata hii ya Chiola, walimu wetu si wangepumua na kujionea fahari taaluma yao! Tuzinduke tusaidiane.

No comments:

Post a Comment