Tuesday, 7 May 2013

Ushirikisha wasababisha shule kufungwa Mbeya

SERIKALI wilayani Kyela kupitia Idara ya Elimu imetangaza kuifunga Shule ya Msingi Kilasilo iliyopo Kata ya Ikimba kutokana na kukithiri kwa vitendo vinavyodhaniwa kuwa vya kishirikina vinavyosababisha shule hiyo pamoja na nyumba za walimu kuwaka moto wa ajabu wakati wa usiku.

Mwenyekiti wa Kijji cha Kilasilo, Fillipo Mwambela, ambaye alidai chanzo cha tatizo hilo ni baada ya kuletwa walimu tisa wa mazoezi shuleni hapo wakitokea Chuo cha Ualimu Mpuguso, wilayani Rungwe.

Alisema baada ya walimu hao kufika, serikali ya kijiji kwa kushilikiana na uongozi wa shule walitoa jengo moja jipya lililojengwa kwa nguvu za wananchi lenye vyumba vitatu kwa lengo la kukaliwa na walimu hao na wengine ambao hawajaripoti.

Baada ya walimu hao kukabidhiwa jengo hilo na kupata kadhia hiyo wakati wa usiku, walitoa taarifa kwa uongozi wa shule na baadaye serikali ya kijiji ambayo iliitisha mkutano wa dharura na wazee wa kimila walikemea na kudai kuwa kama tatizo hilo litaendelea tena watamtaja anayefanya mambo hayo.

Aliendelea kusema usiku wa siku hiyo mambo yalizidi kuwa makubwa, hali iliyowalazimu walimu hao kuikimbia na kwenda kuomba hifadhi nyumba za jirani.

Kaimu Ofisa Elimu Msingi wa Wilaya, Kassim Mtili, mbali na kukiri kuwepo kwa tatizo hilo pia aliwataka wananchi kuacha kujihusisha na vitendo vya kishirikina na badala yake wajikite kuwekeza katika elimu kwa kuwasomesha watoto wao.

Alisema tatizo hilo si la kwanza, kwani katika siku za hivi karibuni kulikuwapo na tatizo la wanafunzi kuanguka na kupoteza fahamu.

No comments:

Post a Comment