Sunday 3 November 2013

Dk Slaa aponda mfumo mpya wa ufaulu

Dk Slaa
SIKU tatu baada ya serikali kutangaza mfumo mpya wa madaraja ya ufaulu, licha ya kupingwa na wengi, kitendo hicho pia kimemhuzunisha Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa.

Akizungumza na gazeti hili jana, Dk. Slaa alisema:  “Kwa kubadili mfumo wa maksi serikali sasa bila huruma imeamua kwa makusudi kabisa kuua ubora wa elimu nchini, ni kweli kwa kupanua wigo wa kufaulu serikali haitalaumiwa kwa akili ya kawaida, itaonekana  wamefaulu wote, lakini elimu haitawasaidia watoto wenyewe, haitawasaidia wazazi wenyewe,  na haitasaidia taifa letu. Tutapataje madaktari bora, tutapataje wanasayansi, walimu au wahandisi bora?  Mabadiliko yanahitajika kusaidia taifa hili lisizikwe na watu wasio na huruma.”

Kwa upande wake, Dk. George Kahangwa, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam akizungumza kupitia kipindi cha ‘Tuongee’ kinachorushwa na Star TV,  alisema  hatua ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Profesa Sifuni Mchome, kutangaza mageuzi hayo ni kuonesha ni jinsi gani serikali  imeshindwa kutatua mzizi  wa tatizo la elimu nchini na baadala yake inatapatapa kwa kuja na sera iliyoiacha kuitumia toka mwaka 1995 iliyotumia alama hiyo ya 50 kwa 50  kwa Tanzania Bara na 40 kwa 60, kwa Visiwani Zanzibar ambapo safari hii imeamua kuitumia tena na kuiweka wazi.

Dk. Kahangwa alisema serikali licha ya kutoa tamko la kubadilisha daraja jipya huku ikikiri kuwa ilikuwa ikitoa alama za kuanzia 75 hadi 100 ndio ufaulu wa alama ‘A’ na daraja la kwanza, pasipo kuiweka wazi kwa muda mrefu, sasa wameamua kuiweka wazi, huku ni kuwaada Watanzania kwa kutumia sera ambayo hazitekelezeki.

“Hili ni janga la elimu, huko nyuma waliondoa ‘sifuri’ kwenye ufaulu na kuweka ‘feli’, leo hii wanakuja tena na kuongezea daraja la tano na kuita ‘ufaulu hafifu au ufaulu usioridhisha’, huku ni kucheza na masuala ya msingi katika taifa. Kuja mbele za umma na kutangaza tena juu ya sera hiyo waliyoiacha kwa muda pasipokuitumia ni jinsi gani sera hiyo haitekelezeki tena,” alisema Dk. Kahangwa.

Dk. Kahangwa amewaomba Watanzania na wadau wa habari nchini kujitokeza kuwahoji wadau wa elimu kama walishirikishwa kwenye kupitishwa kwa mabadiliko hayo.

Dk. Kahangwa alisema  hivi karibuni kuna shirika lilifanya utafiti wa shule za sekondari 100 ambapo shule nne tu ndizo zinahesabika kama shule bora huku 96 zikihesabika kama makambi ya shule.

Hata hivyo, Mhariri Mtendaji wa gazeti la Tanzania Daima, Ansbert Ngurumo, aliyekuwapo kwenye mahojiano hayo alifananisha kitendo cha serikali kupanga madaraja hayo kuwa ni sawa na kupanua magoli ya uwanja ili kila mchezaji afunge, huku akiitaka serikali iwaombe radhi wananchi kwa kuwa ilianza kutumia mfumo huo bila kuwaarifu.

Naye Mratibu wa Chama cha Waandishi wa Habari mkoani Mwanza, Edwin Soko, alisema mabadiliko haya yaliyolenga kuongeza idadi ya wahitimu bila kuangalia uzoefu, yamesababisha taifa kukosa falsafa na Dira ya Taifa.

No comments:

Post a Comment