Picha haihusiani na habari hii |
Tukio hilo limetokea juzi ambapo wanafunzi
hao wanadai kufungiwa katika chumba hicho na Mwalimu Mkuu wa Shule
hiyo, kuanzia saa 2:00 asubuhi hadi saa 7:00 mchana.
Wanafunzi hao wanadaiwa ada kati ya Sh.
50,000 hadi Sh. 400,000. Ada ya mwaka katika shule hiyo kwa mwanafunzi
mmoja ni Sh. 1,300,000.
Wazazi wa wanafunzi hao wakizungumza na
NIPASHE jana mjini Kibaha, walisema walipewa taarifa na watoto wao
kwamba walifungiwa ndani ya chumba kwa sababu hawajalipa ada ya shule,
jambo ambalo limewasikitisha sana na kinyume na haki za binadamu.
“Ukatili waliofanyiwa watoto wetu katika
shule hii haujatufurahisha kabisa, kwani shule hii ni ya kidini sasa
inakuaje Mwalimu Mkuu anakosa roho ya subira,” walisema wazazi hao ambao
walikuwa wamejikusanya kutafakari kwa kina jambo hilo.
Walisema baada ya kupata taarifa kwa barua
kutoka kwa uongozi wa shule kwamba wanatakiwa kuwalipia ada watoto wao,
waliomba wawasilishe ada hiyo wiki ijayo lakini wameshangazwa na
kitendo cha uongozi cha kukosa subira na kuamua kuwafanyia kitendo cha
ukatili watoto wao.
“Ada yenyewe tunayodaiwa tulipe imetokana
na ongezeko la ada kutoka Sh. 850,000 tuliyokuwa tukilipa awali na
kufikia Sh. 1,300,000 kwa mwaka ambayo imepandishwa ghafla, kwanza
watoto wenyewe wanapewa chai ya rangi na mikate tu saa 4:00 asubuhi,”
walisema wazazi hao waliokuwa na jazba.
Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo, Sista Fabiola
alipoulizwa kuhusu madai hayo alisema si ya kweli kwa sababu shule haina
chumba cha kuweza kuwafungia wanafunzi hao kama inavyodaiwa na wazazi.
Alisema wapo watoto ambao wanadaiwa ada
toka Januari hawajalipa na wazazi wao wamekuwa wakipewa barua mara kwa
mara kila shule inapofungwa na kufunguliwa, lakini baadhi yao wamekuwa
wakorofi.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
No comments:
Post a Comment