Sunday 3 November 2013

Matokeo darasa la 7 yatia fora


Baadhi ya wanafunzi hao walipokuwa wakifanya mtihani huo hivi karibuni.
Wakati wanafunzi wa Kidato cha Nne wakianza mitihani yao kesho, Baraza la Mitihani la Tanzania  (NECTA) limetangaza matokeo ya darasa la saba mwaka huu.
Matokeo hayo yanaonesha ufaulu umeongezeka kwa asilimia 19. 89, tofauti na ilivyokuwa mwaka jana.
Katika matokeo hayo, wanafunzi 13 wamefutiwa matokeo, kutokana na udanganyifu ambapo watano walikariri mtihani kwa kufanya mara tatu mwaka 2011, 2012 na mwaka huu. Wengine nane walikutwa na vikaratasi vya majibu katika chumba cha mitihani.
Kaimu Katibu Mtendaji wa Baraza hilo, DK Charles Msonde alitangaza matokeo hayo jana.
Alisema jumla ya watahiniwa 427,606, kati ya 844,938 waliofanya mtihani, wamepata alama zaidi ya 100 katika alama 250, idadi ambayo ni sawa na asilimia 50.61.
Alisema kati yao, wasichana ni 208,227 ambao ni sawa na asilimia 46.68 na wavulana ni 219,379 sawa na asilimia 55.01 huku miongoni mwao wamo wenye ulemavu 476, wasichana wakiwa 219 na wavulana 257.
“Mwaka jana asilimia ya watahiniwa waliopata alama zaidi ya 100 ilikuwa 30.72, hivyo kuna ongezeko la asilimia 19.89 huku takwimu za masomo zikionesha ufaulu katika masomo yote, umepanda kwa asilimia 6.01 na 28.06, ikilinganishwa na mwaka jana,”alisema.
Alibainisha kuwa watahiniwa wamefaulu zaidi katika somo la Kiswahili, ambapo ufaulu ni asilimia 69.06.  Somo walilofaulu kwa kiwango cha chini ni Hisabati, lenye ufaulu wa asilimia 28.62.
Msonde alisema matokeo ya mwaka huu yamewahi, kutokana na watahiniwa kufanya mitihani kwa mara ya pili kwa kutumia Karatasi Maalum za Optical Mark Reader (OMR), ambazo zilisahihishwa kwa kutumia mfumo wa kompyuta.
Alisema washiriki 301 walishiriki katika usahihishaji, ikilinganishwa na washiriki zaidi ya 4,000 waliokuwa wakishiriki kabla ya kuanza kwa mfumo huo. Kwa mwaka huu, usahihishaji umefanywa kwa siku 16, ukilinganishwa na siku 30 zilizotumika awali.
Dk Msonde alisema ili kuhakiki usahihishaji kwa kutumia mfumo wa kompyuta, sampuli ya karatasi 20,795 za majibu kutoka shule 200 katika wilaya 48 za mikoa tisa, zilisahihishwa kwa mkono na kufanyiwa ulinganifu na kusahihishwa kwa kompyuta.
Alisema usahihishaji wa kompyuta, ulikuwa sahihi huku usahihi wa kutumia kalamu ukiwa na makosa ya kibinadamu katika karatasi 249, sawa na asilimia 1.2.
DK Msonde alisema jumla ya watahiniwa 867,983 wa shule za msingi, walisajiliwa kufanya mtihani huo, wakiwemo wasichana 455,896 sawa na asilimia 52.52 na wavulana 412,089 sawa na asilimia 47.48. Kati ya hao, watahiniwa 597 walikuwa wenye uono hafifu na watahiniwa 88 walikuwa wasioona.
Alisema watahiniwa 844,000, sawa na asilimia 97.34 ya waliosajiliwa, walifanya mitihani, kati yao wasichana walikuwa 446,115 sawa na asilimia 97.85 na wavulana 398,823 sawa na asilimia 96.78 .
Alisema watahiniwa 23,045 sawa na asilimia 2.66, hawakufanya mtihani, kutokana na sababu mbalimbali, zikiwemo utoro na ugonjwa. Kati yao, 9,781 sawa na asilimia 2.15 ni wasichana na 13,264  sawa na asilimia 3.22 ni wavulana.
Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Shule na Vyuo Binafsi Tanzania (TAMONGSCO), Mahmoud Mringo alisema shule binafsi zimeongoza katika matokeo hayo kwa kila somo.
Alisema katika somo la Kiswahili, shule binafsi wamepata asilimia 98 wakati za Serikali asilimia  68, na kwa Kingereza shule binafsi asilimia 99 na Serikali 33.
Kwa somo la Maarifa ya Jamii, shule binafsi asilimia 86 Serikali 52 , Hisabati shule binafsi asilimia 81 na Serikali 27 na somo la Sayansi, shule binafsi asilimia 84 na Serikali 46.

No comments:

Post a Comment