CHUO cha Uhifadhi na Usaimamizi wa Wanyamapori, Mweka cha mkoani Kilimanjaro kimesherehekea miaka 50 tangu kuanzishwa kwake kwa kukwama kuendesha harambee kama ilivyopangwa.
Harambee hiyo ilikuwa ifanyike chuoni hapo juzi baada ya kumalizika kwa mkutano wa wataalamu wa usimamizi na uhifadhi wa wanyamapori kutoka nchi za Scandinavia, Bara la Ulaya, Amerika na Afrika, ilikuwa na lengo la kuchangisha kiasi cha dola milioni 3.6 za Marekani kwa ajili ya upanuzi wa chuo hicho.
Kwa mujibu wa ratiba ya shughuli hiyo ya harambee, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alitarajiwa kuwa mgeni rasmi huku uongozi wa chuo hicho ukiwaalika wageni wengine mashuhuri akiwemo waziri mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa na Mwenyekiti wa kampuni za IPP, Reginald Mengi.
Katika hali isiyo ya kawaida hadi muda wa kuanza kwa shughuli hiyo saa saba mchana hakukuwa na mgeni hata mmoja kati ya walioalikwa aliyewasili chuoni hapo na badala yake walionekana walimu na wanachuo tu.
Wakati hali ikiwa hivyo, katika uwanja wa michezo wa chuo hicho ambako kulipambwa kwa ajili ya tukio hilo licha ya kutokuwepo kwa wageni waalikwa Tanzania Daima Jumapili lilishuhudia viti vikiwa wazi licha ya uwepo wa vifaa vya muziki vilivyokuwa vikipiga muziki na matangazo yakiita watu uwanjani hapo.
Hata hivyo ilipotimu saa 8 mchana aliwasili Mbunge wa Kahama, James Lembeli na Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe aliyedaiwa kumwakilisha Pinda.
Baada ya kuwasili Maghembe alipokewa na wafanyakazi wa chuo hicho akiwamo Kaimu Mkuu wa Chuo, Dk. Freddy Manonge, aliyeambatana naye hadi ofisi kuu ya chuo kwa ajili ya kupatiwa maelezo mafupi.
Mazungumzo kati ya Waziri Maghembe na uongozi wa chuo yalichukua muda mrefu, hali iliyolazimu gazeti hili kutaka kujua nini kinaendelea na baada ya kufika katika ofisi hiyo mmoja wa wafanyakazi wa chuo hicho alijibu kwa kifupi: ‘Kuna kikao tutawaita’.
Baada ya kusubiri hadi saa 11 jioni, Lembeli ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge inayoshughulikia Maliasili na Utalii alitoka ndani ya ofisi hiyo kisha akatoka makamu mkuu wa chuo akiambatana na Ofisa Uhusiano wa chuo hicho, Richard Kisasembe.
Mkuu wa chuo hicho baada ya kufanya mawasiliano na mshereheshaji wa shughuli aliyefahamika kwa jina moja la Peter baadaye alitoa tangazo la mabadiliko akisema kutokana na watu wengi waliokuwa wamealikwa kupata dharura hivyo shughuli ya harambee imehairishwa.
“Baada ya watu wengi kupata dharura wale ambao tumekuja leo kwa ajili ya kuchangia basi tunaomba waende ofisini ili kwenda kutoa ahadi zenu pale na kesho (jana) tutatangaza kiasi kilichopatika kwa hiyo suala la harambee tutalikamilisha kesho,” alisema mshereheshaji Peter.
Akizungumzia hali hiyo, Profesa Maghembe alisema alimwakilisha Waziri Mkuu Pinda ambaye ametingwa na shughuli za Bunge.
Kuhusu ujangili, Profesa Maghembe alisema lipo tatizo katika nchi za Afrika, wapo watu wenye uchu wa kujipatia mali kwa haraka, ambao wanataka kumaliza rasilimali za wanyamapori waliotunzwa kwa ghamara na muda mrefu.
TANZANIA DAIMA
No comments:
Post a Comment