JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA ELIMU NA MAFUNZO YA UFUNDI
Wizara
imekusanya maoni ya Wadau wa Elimu kuhusu Upangaji wa Viwango vya Alama
(Grade Ranges) katika Mitihani ya Kuhitimu Kidato cha Nne na cha Sita
pamoja na Matumizi ya Alama za Tathmini Endelevu ya Mwanafunzi
(Continuous Assessment ama CA) kwa ajili ya kuamua kiwango cha ufaulu wa
mwanafunzi. Maoni ya wadau yamekusanywa kwa sababu kwa muda mrefu sasa
upangaji wa viwango vya alama vinavyotumika na utaratibu wake katika
mitihani ya kuhitimu Kidato cha Nne na Kidato cha Sita umekuwa haufanani
pamoja na kwamba mitihani hiyo yote ni ya elimu ya sekondari. Pia mfumo
masuala mbalimbali ya mitihani katika elimu ya sekondari umekuwa na
miundo tofauti ikiwemo ule unaotumika shuleni na ule wa Baraza la
Mitihani la Taifa. Kwa sasa kuna miundo mikuu miwili katika mfumo huo.
Muundo
wa Kwanza ni upangaji wa viwango katika ngazi ya Shule ambapo Alama
Mgando (Fixed Grade Ranges) zifuatazo hutumika kupanga madaraja: A = 81 –
100; B = 61 – 80; C = 41 – 60; D = 21 – 40 na F = 0 – 20. Muundo huu
umetumika kwa muda mrefu na umezoeleka kwa walimu na wanafunzi wa elimu
ya sekondari kwa ujumla.
Muundo
wa Pili ni wa viwango vinavyotumiwa na Baraza la Mitihani la Taifa
ambapo ambapo kabla ya mwaka 2012 muundo wa viwango nyumbufu (flexible grade ranges)
ulitumika. Katika muundo huu uwigo wa alama ulibadilika badilika
kulingana na hali ya matokeo ilivyokuwa kwa mwaka husika. Lakini kuanzia
mwaka 2012, Serikali iliamua kutumia mfumo wa Upangaji wa Alama Mgando
(Fixed Grade Range) kwa Kidato cha Nne na Kidato cha Sita. Katika
mtihani wa Kidato cha Nne mwaka 2012 Baraza lilitumia mfumo huu wa alama
mgando ambapo: A = 80 – 100, B = 65 – 79, C = 50 – 64, D = 35 – 49, F =
0 – 34. Kwa upande wa Kidato cha Sita Baraza lilitumia mfumo wa A = 80 –
100; B = 75 - 79; C = 65 – 74; D = 55 – 64; E = 45 – 54; S = 40 – 44 na
F = 0 – 39. Mifumo hii ya Baraza haikuwa inafahamika kwa wadau na hivyo
kuwa sehemu ya malalamiko katika sekta ya elimu na mafunzo.
Vilevile,
Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 1995 imeelekeza kwamba katika kuamua
kiwango cha ufaulu wa mwanafunzi wa elimu ya sekondari, Alama za CA
zitachangia asilimia hamsini (50%) na Mtihani wa mwisho utachangia
asilimia hamsini (50%). Kwa upande wa Zanzibar, CA zimekuwa zikiandaliwa
kwa mfumo wa asilimia arobaini (40%) na mtihani wa mwisho asilimia
sitini (60%). Pamoja na kwamba Baraza halijawahi kuutumia mifumo hii
tangu ilipowekwa, kumekuwa na mitazamo, maoni na mapendekezo tofauti
katika muundo na matumizi ya alama za CA. Kuna mawazo pia kwamba mfumo
wa CA kuchangia matokeo ya mwisho ya mwanafunzi pia utumike kwa
watahiniwa wa kujitegemea (private candidates).
Kwa
sasa matokeo ya mitihani ya watahiniwa hawa yamekuwa yakitumia alama za
mtihani wa mwisho tu na hivyo kutafsiriwa kama utaratibu ambao
unamwonea mwanafunzi ambaye anahamu ya kujiendeleza kielimu lakini
anakwama kwa sababu mfumo unaotumika siyo rafiki kwa mtahiniwa.
Kwa mantiki hii, Wizara imedhamiria kufanya harmonization ya
masuala ya alama katika mitihani ya Kidato cha Nne na Kidato cha Sita
ili kupata muundo mmoja na ulio wazi kwa wadau wote wa elimu ya
sekondari. Lakini pia serikali imedhamiria kuhakikisha tathmini za
wanafunzi katika ngazi mbalimbali zinakwenda sambamba na matarajio ya
mitaala inayotumika na ambayo inahuishwa mara kwa mara ili iendane na
wakati na mahitaji ya elimu katika ngazi mbalimbali.
VIWANGO NA UTARATIBU KUANZIA MWAKA 2013 KWA KIDATO CHA NNE NA MWAKA 2014 KIDATO CHA SITA
Baada
ya kufanya tathmini ya maoni mbalimbali ya wadau, misingi ifuatayo
ilizingatiwa katika maamuzi kuhusu makundi ya alama na muachano wake:
a) Alama zitakazotumika zitakuwa A, B, C, D, E na F.
Muachano wa alama kati ya kundi moja hadi jingine utafanana, isipokuwa
tu pale ambapo itaonekana kuna sababu na hakuna athari za kuwa na
muachano tofauti na ule ambao umetumika katika makundi mengine.
b) Makundi ya alama hayatakuwa na clusters isipokuwa
pale ambapo itaonekana kufanya hivyo kunaleta tija katika kupata picha
ya wahitimu kwa ajili ya matumizi mbalimbali. Kwa mantiki hii
(i) makundi ya alama A, C, D, E na F yabaki na cluster moja moja bali kundi la alama Blitakuwa na clusters mbili.
Kundi la kwanza litakuwa la wale ambao wamepata alama kati ya 50 mpaka
59 na litaitwa B na lingine litakuwa la wale ambao wamevuka uwigo wa 50
hadi 59 na kuelekea uwigo wa 60 hadi 74 na hili litaitwa B+ (angalia
jedwali hapo chini).
(ii) Pamoja na kuwa na muachano wa alama 26 kama jedwali linavyoonesha hapo chini, alama A kwa
miaka mingi imekuwa ikianzia alama 75 hadi 100 na kwamba pamoja na
uwigo huo bado wanaofaulu kwa kiwango hicho ni wachache sana. Kwa
mantiki hii, hakuna haja ya kubadilisha uwigo ila juhudi ziendelee
katika ufundishaji na ujifunzaji ili kiwango cha ufaulu kiongezeke na
kupata wanafunzi wengi zaidi wanaofaulu katika kundi hili.
(iii)
Pia, pamoja na kuwa na muachano wa alama 20 kama jedwali
linavyoonesha hapo chini kwa miaka mingi, huko shuleni mwanafunzi
aliyepata alama 21 na hadi 30 alihesabiwa kuwa na ufaulu wa chini kabisa
au hafifu kwa kiwango cha alama D na ingawa ilikubalika ufaulu wa aina hiyo kwa mazingira ya nchi yetu unaridhisha. Alama F ilikuwa ni kwa wale waliopata chini ya hapo. Hivyo, alama F itaendelea kuwepo na itaanzia alama 0 hadi 19 na E itaanzia alama 20 hadi 29 na D –
30 -39. Lengo la muundo huu ni kuwa alama mbalimbali, isipokuwa kwa
makundi machache, zianzie kwenye 0 yaani 0, 10, 20, 30, 40 na kuendelea
badala ya kuanzia kwenye moja yaani 1, 11, 21, 31, 41 na kuendelea. Hii
ni kwa ajili ya kuleta mtizamo unaofanana katika ngazi mbalimbali za
elimu ambapo kwa sasa ngazi ambazo siyo za elimu msingi na sekondari
zinatumia muundo wa kuanzia kwenye 0 badala ya 1.
c) Uwigo
wa jumla wa alama kwa Kidato cha Nne na Kidato cha Sita utaendelea kuwa
wa alama 0 hadi 100 na kila kundi katika uwigo huu limepewa tafsiri kwa
ajili ya kuamua mambo mbalimbali yanayohusu maendeleo ya mwanafunzi
kulingana na malengo ya mtihani husika. Kimsingi, tafsiri zifuatazo
zitakatumika
(i) Alama A itakuwa na maana ya ufaulu uliojipambanua (distincion or outstanding performance),
(ii) Alama B+ itakuwa na maana ya ufaulu bora sana (excellent performance),
(iii) Alama B itakuwa na maana ya ufaulu mzuri sana ( very good perfomance),
(iv) Alama C itakuwa na maana ya ufaulu mzuri (good performance);
(v) Alama D itakuwa na maana ya ufaulu wa wastani (low performance),
(vi) Alama E itakuwa na maana ya ufaulu hafifu (very low performance), na
(vii) Alama F itakuwa na maana ya ufaulu usioridhisha (unsatisfactory performance).
Wataalamu
katika maeneo mbalimbali ya elimu na ulimwengu wa kazi, kwa
kushirikiana na Wizara, watatoa maana ya tafsiri hizi kiutendaji katika
maeneo yao kulingana pia na mahitaji yao.
d) Alama C iwe ndiyo alama ya ufaulu mzuri ambao hauhitaji urekebu wa lazima, wakati alama D na E ni
alama za ufaulu unaohitaji urekebu kadri mwanafunzi atakavyokuwa
anaendelea na masomo ili kuthibitisha kama mlengwa anaweza na kulingana
na mahitaji ya eneo husika (targeted remediation). Alama F iwe alama ya eneo linalohitaji urekebu wa hali ya juu (intesive remediation) ili mwanafunzi huyo aweze kumudu masomo kadri anavyoendelea kukua kielimu ama atakapoingia katika ulimwengu wa kazi.
e) Makundi ya alama yatajumuisha CA kwa
kiwango cha asilimia isiyozidi 40 na mtihani wa mwisho kwa asilimia
isiyozidi 60 kwa makundi yote ya watahiniwa ikiwemo wale wa kujitegemea (private candidates). Hii ni kwa kuzingatia kwamba CA siyo vizuri izidi uwigo wa alama ya ufaulu mzuri unapoanzia ambayo ni C au 40.
f) CA kwa
upande wa Kidato cha Nne zitokane na mtihani wa Kidato cha Pili (alama
15), matokeo ya Kidato cha Tatu (alama 5 kwa kila muhula, na hivyo
jumla ya alama 10), mtihani wa Mock (alama 10) na kazi mradi auProjects (alama 5). Kwa upande wa Kidato cha Sita, CA iendelee kutokana na muundo unaotumika sasa.
g) CA zitumike pia kwa watahiniwa wa kujitegemea. Kwa upande wa watahiniwa wa kujitegmea ambao wanarudia Mitihani, CA zao
zitumike zile zilizotumika kutoa matokeo yake ya mitihani ya awali.
Kwa watahiniwa wa kujitegemea waliopitia mfumo wa Qualifying Test (QT), matokeo ya QT yatumike kama CA na mtihani wa mwisho uchangie alama 60.
h) Kwa
vile alama endelevu kwa mwaka 2013 kwa wanafunzi wa Kidato cha Nne
tayari zimeshawasilishwa Baraza la Mitihani Tanzania, alama hizo
zichangie asilimia 40 katika mtihani wa Kidato cha Nne mwaka 2013.
i) Muundo wa wastani wa alama katika ufaulu (Grade Points Average ama
GPA) utaandaliwa na kuanza kutumika pale utakapokuwa tayari na wadau
wataelimishwa kuhusu muundo huo ili wapate kuufahamu na manufaa yake
katika elimu ya sekondari.
j) Muundo
huu mpya wa alama utatumika kwa mzunguko wa miaka minne kabla
haujahuishwa tena ili kuupa muda wa kutosha kuona aina ya changamoto
zinazojitokeza na jinsi ya kuzishughulikia. Aina hii ya muda itaruhusu
vidato vinne vya elimu ya sekondari ya kawaida na nane ya elimu ya
sekondari ya juu kupimwa. Hata hivyo, uhusihaji wa masuala ya mitihani
unaweza ukafanyika iwapo matokeo ya uhuishaji wa mitaala kwa ujumla
utahitaji pia eneo la mitihani liguswe na kuhuishwa pia.
Kwa mantiki hii, viwango vya alama na ufaulu ni kama inavyooneshwa kwenye jedwali la 1 hapa chini:
Jedwali Na 1
MUUNDO WA ALAMA NA UFAULU
ALAMA
|
UWIGO WA ALAMA
|
IDADI YA ALAMA
|
TAFSIRI
|
A
|
75 - 100
|
26
|
Ufauli Uliojipambanua
|
B+
|
60 - 74
|
15
|
Ufaulu bora sana
|
B
|
50- 59
|
10
|
Ufaulu mzuri sana
|
C
|
40 - 49
|
10
|
Ufaulu mzuri
|
D
|
30 - 39
|
10
|
Ufaulu Hafifu
|
E
|
20 - 29
|
10
|
Ufaulu hafifu sana
|
F
|
0 - 19
|
20
|
Ufaulu usioridhisha
|
Kwa
aina hii ya muundo wa alama, na kwa kuwa muundo wa GPA utaanza
kuandaliwa na wadau kuelimishwa kabla haujaanza kutumika, katika kipindi
hiki mpaka wakati huo, muundo wa madaraja utakuwa kama inavyooneshwa
kwenye jedwali la 2 hapa chini.
Jedwali Na 2
MUUNDO WA MADARAJA
MUUNDO WA ZAMANI
|
MUUNDO MPYA
|
MAELEZO
|
POINTI
|
DARAJA
|
POINTI
|
DARAJA
|
7-17
|
1
|
7-17
|
I
|
Kundi la ufaulu uliojipambanua na bora sana
|
18-21
|
II
|
18-24
|
II
|
Kundi la ufaulu mzuri sana
|
22-25
|
III
|
25-31
|
III
|
Kundi la ufaulu mzuri na wa wastani
|
26-33
|
IV
|
32-47
|
IV
|
Kundi ufaulu hafifu
|
34-35
|
0
|
48-49
|
V
|
Kundi la ufaulu usioridhisha
|
Wataalamu
wa mifumo ya mitihani watalifanyia kazi zaidi jedwali hili la madaraja
ili liweze kutumika kwa ufanisi katika kipindi hiki cha mpito.
Kwa
mantiki hii, Daraja Sifuri linafutwa na kuwekwa daraja litakalojulikana
kama Daraja la Tano na ambalo litakuwa ndilo la mwisho kabisa katika
ufaulu.
HITIMISHO
Mabadiliko
haya yamefanyika ili kuendelea kuimarisha mfumo wetu wa elimu na kuweka
wazi taratibu mbalimbali kwa ajili ya mitihani na masuala mengine. Yako
mambo mengi mengine ambayo hayana budi kuendelea kuimarishwa ikiwemo
mfumo wa mitaala, walimu, mazingira ya kujifunzia na kufundishia pamoja
na vitabu na vifaa vingine muhimu katika elimu. Masuala haya yanaendelea
kuangaliwa kupitia mikakati mbalimbali ikiwemo mpango wa Matokeo
Makubwa Sasa ama Big Results Now (BRN). Ushirikiano wa wadau wote
ili kuleta tija kwenye elimu ni muhimu sana na hivyo wizara itaendelea
kuwashirikisha wadau wote kwa kadri itakavyohitajika na wadau pia
wanaombwa wasiache kuishirikisha wizara pale watakapokuwa na jambo
lolote ambalo linahitaji ushirikiano ili kwa pamoja tuweze kupata
mafanikio katika sekta ya elimu.
Imetolewa,
KATIBU MKUU
WIZARA YA ELIMU NA MAFUNZO YA UFUNDI