Friday, 17 May 2013

Dk Hosea aichangia Shule ya Sekondari Sh Mil. 10

http://3.bp.blogspot.com/-_zulXoZDlto/UGp3VbIUgQI/AAAAAAAAJCw/IhvsYRq0XCE/s1600/6.jpeg
Dk Hosea


MKURUGENZI Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini Dk. Edward Hosea ametoa sh milioni 10 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya maabara katika shule ya sekondari ya Binza iliyoko wilayani Maswa, Simiyu.

Akikabidhi fedha hizo jana kwa niaba yake Katibu Tawala wa wilaya ya Maswa, Danford Peter, mbele ya wanafunzi na walimu wa shule hiyo katika sherehe iliyofanyika shuleni hapo alisema hiyo ni utekelezaji wa ahadi aliyoitoa mwaka jana alipokutana na wazee wa mji huo.

Alisema kuwa Desemba 25 mwaka jana Dk. Hosea alikutana na baadhi ya wazee wa Nyalikungu yalipo makao makuu ya wilaya hiyo na mambo mengine walimwomba kusaidia ununuzi wa vifaa vya maabara katika shule hiyo.

“Dk. Hosea alipofika hapa kwa ajili ya mapumziko ya sikukuu ya Krismasi mwaka jana alionana na wazee wa mji huu na mazungumzo mengine walimwomba kusaidia ununuzi wa vifaa vya maabara na leo ametimiza ahadi yake na tunakabidhi hundi ya sh milioni 10 kwa uongozi wa shule ya Binza,” alisema.

Alisema kuwa kupatikana kwa vifaa hivyo kutawasaidia wanafunzi hao kujifunza kwa vitendo masomo ya sayansi ambayo mara nyingi hawayapendi kutokana na kutokuwepo kwa vifaa vya maabara.

Naye mkuu wa TAKUKURU wilayani hapa Daniel Ntera aliutaka uongozi wa shule hiyo kuzitumia fedha hizo kama ilivyokusudiwa na kwamba ofisi hiyo itafuatilia.

Akipokea hundi hiyo, mkuu wa shule ya Binza, Focus Nshiyiki, alimshukuru Dk. Hosea na kuahidi kuzitumia fedha hizo kama ilivyokusudia kwa kufuata kanuni, taratibu na sheria za manunuzi ya umma.

Wanafunzi zaidi ya 7000 waliofaulu wakacha shule Karagwe

http://www.ippmedia.com/media/picture/large/dc.jpg
Mkuu wa Wilaya ya Karagwe, Darry Rwegarira
JUMLA ya wanafunzi 7,338 hawakujiunga katika shule mbalimbali za sekondari za kata wilayani Karagwe, Kagera katika kipindi cha mwaka 2010 hadi 2012.

Mkuu wa Wilaya ya Karagwe, Darry Rwegasira alibainisha hayo jana alipokuwa akiwatuhumu madiwani wa halmashauri hiyo kwenye Ukumbi wa Rafiki wa Angaza uliopo wilayani hapa.

Alisema wanafunzi hao hawakujiunga na elimu ya sekondari pamoja na kufaulu mtihani wa taifa katika kipindi hicho.

“Tuwaandalie watoto wetu urithi wa elimu kuliko tabia zilizopo za kuchangia harusi na kuwasahau watoto ambao ndio watakaolikomboa taifa hili kwa nyanja zote,” alisema Rwegasira.

Alibainisha katika mwaka 2010 wanafunzi waliochaguliwa walikuwa 5,150. Kati ya hao 1,177 hawakuripoti shuleni, mwaka 2011 wanafunzi 5,107 walichaguliwa na 2,155 hawakuripoti shule na katika mwaka 2012 kati ya 8,871 wanafunzi 4,006 hawakuripoti shuleni.

Hata hivyo, alisema shule nyingi za sekondari katika wilaya hiyo hazina miundombinu iliyodumu kutokana na baadhi ya wazazi kutokuwa na mwamko wa kuchangia maendeleo ya shule na kuongeza kuwa kata ambazo hazina sekondari za kata zimekuwa na tatizo katika kuchangia maendeleo ya shule za kata zilizo jirani.

CWT yaonywa na Asasi wa Wataalamu wa Ualimu

http://in2eastafrica.net/wp-content/uploads/2012/03/Gratian-Mukoba.jpg
Rais wa CWT, Gratian Mukoba
TAASISI ya Mtandao wa Wataalamu wa Ualimu Nchini (TTN) unaoshughulikia masuala ya sheria, imekionya Chama cha Walimu Tanzania (CWT) kufuata taratibu na sheria zote ili kumnufaisha mwalimu.

Onyo hilo lilitolewa jana na Mwenyekiti wa TTN, Faray Alfred, alipozungumza na waandishi wa habari jijini Mwanza kuhusiana na ukiukwaji wa sheria unaofanywa na CWT dhidi ya mwalimu.

Alfred alisema tangu CWT isajiliwe kisheria miaka ya 1992, imekuwa ikikiuka baadhi ya sheria za mfanyakazi wa taaluma ya ualimu, hivyo kusababisha walimu wengi kutonufaika na kazi ya chama hicho cha walimu.

Alisema tangu kuanzishwa kwake hadi sasa, CWT haiweki wazi mapato na matumizi kwa wanachama wake, ikiwa ni pamoja na kutokuwa na takwimu halisi za walimu ambao ni wanachama hai na mawakala wa ada, jambo linalotilia shaka uendeshwaji wa chama hicho.

“Uchunguzi uliofanywa na TTN umebaini CWT inakiuka sheria nyingi za nchi na Katiba ya Jamhuri ya Muungano. Kwanza inamkata mwalimu ada ya asilimia mbili pale anapoajiriwa bila ridhaa yake.

“Pili, CWT hawana mfumo wa kueleza mapato na matumizi, wala hawawaelezi wanachama wao kuhusu matumizi. Hili ni tatizo lazima timu ya TTN ambayo imesajiliwa kisheria mwaka jana itoe onyo kwa CWT,” alisema Alfred.

Kwa upande wake, mratibu wa TTN, Tungaraza Njugu alisema kwamba utendaji mbovu wa CWT ndiyo unaosababisha taaluma ya ualimu kushuka, kwani walimu wenyewe wameanza kukata tamaa.

“TTN tumesajiliwa kwa ajili ya kulinda na kutetea haki sheria za walimu. Kwa sasa tunafanya kampeni ya kuwaelimisha walimu jinsi CWT inavyowatendea ndivyo sivyo,” alisema.

Chanzo:Tanzania Daima

Tuesday, 14 May 2013

Wanawake wahimizwa kutumia mitandao kutangaza biashara zao


Mkurugenzi wa kampuni Dare to Dream, Bi Emelda Mwamaga

WANAWAKE wajasiriamali wameshauriwa kutumia mitandao ya kijamii kutangaza biashara zao badala ya kuitumia kufanya mambo yasiyo na maana.

Ushauri huo ulitolewa jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki na Meneja wa Vodacom Foundation, Grace Lyon, katika mkutano wa tano wa uchumi wa wanawake wajasiriamali.

Akizungumza katika mkutano huo uliondaliwa na Kampuni ya Dare To Dream alisema: “Ni vizuri wafanyabiashara wakatumia mitandao ya kijamii ipasavyo katika kutangaza biashara zao sambamba na huduma ya M-pesa kwa ajili ya kuokoa muda wa kupanga foleni kwenye benki, mwanamke mjasiriamali akiwa mtumiaji wa huduma hii anakuwa katika hali ya usalama zaidi kwa fedha zake,” alisema Lyon.

Alisema huduma hiyo hivi sasa imepanuka kiasi cha kutoa huduma zaidi ya 200, hivyo alitumia fursa hiyo kuwahamasisha wanawake wote nchini kujiunga.

Mkutano huo uliowakutanisha wanawake wajasiriamali uliambatana na mafunzo mbalimbali ya kukuza biashara pamoja na maonesho ya bidhaa mbalimbali.

Jinsi Wanamakuka 2013 tulivyoshiriki semina ya wajasiliamali wanawake iliyofanyika jijini Dar

Wanamakuka wenzangu, Aziza Mbogulume na Theonestina wakiwa makini kwenye semina hiyo ya Jumamosi
Hawa ni baadhi ya jopo la waandaaji wa Tuzo ya Mwanamakuka. Wa pili toka kulia ni Bi. Mariam Shamo aliyetuwezesha kuhudhuria semina hiyo.
Mimi na mshindi wa tatu wa tuzo za mwanamakuka Theonestina (kati) na mshindi wa kwanza Aziza Mbogulume (kulia) tukiwa katika pozi.

JUMAMOSI mimi pamoja na Wanamakuka wenzangu tulioshinda mwaka huu wa 2013 tulikuwa miongoni mwa wanawake wajasiriamali tuliohudhuria mkutano na semina ya wajasiriamali iliyoandaliwa na  kampuni ya Dare to Dream na kudhaminiwa na kampuni za Vodacom na Benki ya CRDB.
Ushiriki wetu katika semina hiyo iliyoambatana na maonyesho ya bidhaa za wajasiriamali wenzetu wa ndani na nje ya mkoa wa Dar uliwezeshwa na Mratibu wa Tuzo za Mwanamakuka, Bi. Mariam Shamo kutoka Umoja wa Wanawake Marafiki (UWF).
Kwa hakika tuliweza kujifunza vitu vingi ambavyo kabla ya semina na mkutano huo hatukuwa tunafahamu, hivyo mimi binafsi na kwa niaba ya wanamakuka wa 2013 tunamshukuru mno Bi Mariam na jopo zima la UWF, bila kuwasahau kampuni ya siku Airtel  ambayo ilidhamini zawadi ya ushindi wangu wa pili.

Monday, 13 May 2013

Matokeo mapya kidato cha nne kutangazwa wiki hii

https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEh9sNHa_M6qauWq742O49nDz4wm0dbK0cQ9Wf6vLk9CaGOmKj2icOhyphenhyphennQAqvilezQsA8gXTGo-RrAahPMqn-Q-mIT96dBkBziaXbUeFpDa1uF0fRBEN0Wm2BxwhUDIvVRcZHqa5-Sdnsk2X/s1600/SHUKURUMM.jpg
Waziri wa Elimu n Ufundi Stadi, Dk Shukuru Kawambwa

MATOKEO mapya ya mtihani wa kidato cha nne mwaka 2012 yanatarajia kutangazwa na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi siku yeyote wiki hii.

Kutangazwa upya kwa matokeo hayo kunafuatia uamuzi uliochukuliwa na serikali hivi karibuni kufuta wa matokeo hayo ili yaandaliwe upya kwa kutumia utaratibu uliotumika mwaka 2011.

Habari ambazo NIPASHE imezipata jana na kuthibitishwa na viongozi wandamizi wa wizara hiyo, kazi ya kufanya marekebisho ya matokeo hayo imeshakamilika na yatatangazwa wiki hii.

“Kazi ya kuandaa matokeo imekwishakamilika sababu ni kazi inayofanywa na watu watatu kwa kutumia kompyuta,” alisema ofisa mmoja ambaye alisema taarifa rasmi zitatolewa na Waziri wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa.

Dk. Kawambwa na Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Taifa (Necta),  Dk. Joyce Ndalichako, walipotafutwa kueleza suala hilo jana, simu zao zilikuwa zikiita bila kupokelewa.

Hata Hivyo, Afisa Habari wa Necta, John Nchimbi, alisema mchakato wa kuandaa matokeo hayo unaendelea na kwamba yatatangazwa muda wowote.

Mei 3, mwaka huu serikali ilitangaza kufuta matokeo hayo na kuamua yaandaliwe upya.

Uamuzi huo wa Serikali ambao ulitangazwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, kwamba umetokana na matokeo mabaya ya mitihani huo yaliyosababisha zaidi ya asilimia 60 ya wanafunzi kupata sifuri.

Kutokana na matokeo hayo, Serikali iliunda Tume inayoongozwa na Profesa Sifuni Mchome kuchunguza matokeo hayo ili kupata ufumbuzi wa kudumu.

Katika mtihani wa mwaka 2012, wanafunzi 367,756 walifanya mtihani huo na waliofaulu ni 126,847. Waliofaulu kwa kwa madaraja ya kwanza hadi la tatu ni 23,520 sawa na asilimia 6.4 na daraja la nne ni 103,327 sawa na asilimia 28.1, huku 240,909 ambao ni asilimia 65.5 wakipata daraja sifuri.

CHANZO: NIPASHE

Tundu Lissu ahamasisha wanafunzi kupiga kura 2015


https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEgdf-fs9lRtAbwYc1sx08053pPBXaAQTnKlLQW1Bg_CEMPkk5OaZ8-CBtNfNJla1ddDXmvpfykg35TO_JPc9-dgmErBeIJ8iZJecUeXvkRxbOV7aa-U_xdYBH_kUykKiAv_79hbOxaTdAN7/s1600/tundu-lissu-2.jpg
Mhe. Tundu Lissu

MBUNGE machachari wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (CHADEMA) amewataka wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Mkwawa kutumia kura zao vizuri katika uchaguzi mkuu mwaka 2015 ili kuiondoa madarakani Serikali ya Chama Cha Mapinduzi kutokana na kudidimiza uchumi na kutoleta maendeleo nchini.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara baada ya kualikwa na Jumuiya ya Wanafunzi wa CHADEMA walioko mkoani Iringa, Lissu alisema Serikali ya CCM imeshindwa kumkomboa mwananchi kutokana na wabunge na viongozi wake kutokuwa na uchungu na nchi.

Alisema ni kazi kubwa kwa sasa kwa mwananchi kupata maendeleo chini ya CCM, hivyo ni jukumu la kila mwananchi kuitumia kura yake kuwachagua wabunge wengi wa upinzani na upande wa rais.

“Kila Mtanzania anajua kuwa utawala wa CCM ni giza tupu, angalieni maisha ya walimu, askari, wakulima na wafanyakazi, wako katika hali ngumu sana,” alisema.

Aidha, alitumia nafasi hiyo kumsifu Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa kwa kazi anayofanya katika kutetea maslahi ya taifa na Mkoa wa Iringa kwa ujumla kutokana na kusimama kidete bungeni.

Sunday, 12 May 2013

Wanawake wajasiriamali wana nafasi ya kufanikisha biashara zao

Baadhi ya wafanyakazi wa Vodacom Tanzania walioshiriki katika warsha ya wanawake wajasiriamali wadogo na wa kati, iliyoandaliwa na taasisi isiyo ya kiserikali ya Dare to Dream na kudhaminiwa na Vodacom Tanzania, Benki ya CRDB na kinywaji cha Malta. Warsha hiyo inayofanyika mara moja kwa mwaka ilifanyika jijini Dar es Salaam kwa kuwashirikisha wanawake zaidi ya 150.
Baadhi ya wafanyakazi wa Vodacom Tanzania wakifuatilia moja ya mada zilizokuwa zikitolewa katika warsha ya wanawake wajasiriamali wadogo na wa kati, iliyoandaliwa na taasisi isiyo ya kiserikali ya Dare to Dream na kudhaminiwa na Vodacom Tanzania, Benki ya CRDB na kinywaji cha Malta. Warsha hiyo inayofanyika mara moja kwa mwaka ilifanyika jijini Dar es Salaam kwa kuwashirikisha wanawake zaidi ya 150.
Washiriki wa warsha ya wanawake wajasiriamali wadogo na wa kati, wakifungua warsha hiyo kwa kusali.
Washiriki wa warsha ya wanawake wajasiriamali wadogo na wa kati, wakifungua warsha hiyo kwa kusali.
Mkufunzi na mtaalamu wa maswala ya ujasiriamali, Bi. Rehmah Kasule, akitoa elimu kwa wanawake zaidi ya 150 juu ya kuwawezesha kujua mbinu za kujiendeleza katika kukuza biashara zao.
Msanii wa nyimbo za injili ambaye pia ni mjasiriamali, Bi. Elizabeth Benard, akiimba wimbo wa "anafanya jambo" katika warsha ya wanawake wajasiriamali zaidi ya 150.
Mkurugenzi mtendaji wa Taasisi isiyokuwa ya kiserikali ya Dare to Dream, Bi.Emelda Mwamanga, akifanyiwa mahojiano na waandishi wa habari juu ya warsha ya wanawake wajasiriamali iliyoandaliwa na taasisi yake na kudhaminiwa na Vodacom Tanzania, Benki ya CRDB na kinywaji cha Malta.
Na Mwandishi wetu
WANAWAKE wajasiriamali wa Kitanzania wanayo nafasi nzuri ya kufanikiwa katika biashara zao ikiwa watajiamini na kuwa na uthubutu katika shughuli zao
Akizungumza wakati wa semina ya wanawake wajasiriamali iliyoambatana na maonyesho ya bidhaa mbalimbali jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki, Afisa mtendaji mkuu wa taasisi isiyokuwa ya kiserikali ya Dare to Dream foundation iliyoandaa semina hiyo Emelda Mwamanga alisema kutojiamini ni moja kati ya sababu zinazowafanya wanawake wajasiriamali kushindwa kusonga mbele
Emelda alisema kuwa, duniani ya sasa ya kibiashara imejaa ushindani mkubwa na bila kujiamini itakuwa ni vigumu kwa wanawake wajasiriamali kuweza kufanikiwa.
"Semina hii imewaleta pamoja wanawake wa kada mbalimbali ili kuweza kubadilishana uzoefu pamoja na kutiana moyo. Wapo waliofanikiwa kibiashara ambao watawaeleza wale ambao bado hawajafanikia njia walizopitia mpaka kufika hapo walipo. Kupitia semina hii watajifunza na namna ya kutengeneza bidhaa zenye viwango pamoja na namna ya kujitanga," alisema
Kwa upande wake Afisa masoko wa benki ya CRDB Emmanuel Kiondo alisema kuwa benki yake inatambua umuhimu wa kumwezesha mwanamke na ndiyo maana ikaamua kujitokeza kudhamini shughuli hiyo iliyolenga kuwajengea uwezo wanawake
Tunaamini kuwa mwanamke akiwezeshwa familia nzima inakuwa imewezeshwa. Benki ya CRDB imekuwa ikimjali sana mwanamke na tumeweza kuanzisha akaunti ya Malkia maalumu kwa ajili ya wanawake wenye malengo mbalimbali ikiwemo ya kiujasiriamali," alieleza
Mwakilishi kutoka kampuni ya Vodacom ambao ndiyo wadhamini wakuu wa semina na maonyesho hayo Alice Lewis alisema Vodacom inatambua mchango wa wanawake katika maendeleo ya jamii na itaendelea kuwa mstari wa mbele kuwasaidia kusonga mbele.
Credit: Kapingaz

Multichoice Tanzania kusambaza Digital Shule za Msingi nchini



Meneja Uhusiano wa MultiChoice Tanzania, Barbara Kambogi akiwakaribisha wageni wanahabari katika hafla mchapalo ya kusheherekea Africa Day na Dstv ambapo amesema DStv inatoa nafasi kwa wateja wake kuwa na fursa ya kuchagua vifurushi mbalimbali kulingana na uwezo wa mteja ambacho cha uwezo wa chini kabisa ni Access chenye zaidi ya channeli 40 gharama yake ni nafuu sana ambapo mteja atalipia shilingi 16,500 kwa mwezi. (Picha na Zainul Mzige wa dewjiblog).
Meneja wa Fedha wa kampuni ya Multichoice Tanzania, Bw. Francis Senguji akizungumzia malengo ya DStv Tanzania ambapo amesema wao kama waendeshaji wa biashara nyingine barani Afrika wanaojali na kuthamini maendeleo ya jamii wameona ni wajibu kusaidia jamii ili kuweza kuendeleza maendeleo ya kijamii nchini Tanzania.
Kwa kuendeleza hilo Multichoice ina mfumo wa kutoa elimu mashuleni ( Multichoice Resource Centre) hivyo watamumia jukwaa la Teknolojia kama darasa kwa njia mbalimbali kuwapa jamii nafasi ya kuendeleza vipaji na ujuzi.
Mfumo huo kutoa rasilimali kwenye shule kama vile ving’amuzi vya Satellite, VCRs/DVD na kifurushi cha elimu cha Dstv. Mpaka sasa Multichoice imeanzisha vituo vya rasilimali jamii katika shule 82 nchi nzima kwenye mikoa ya Arusha, Dar es Salaam, Dodoma, Iringa, Kagera, Mbeya, Pwani na Tanga.

Meneja Uendeshaji wa Multichoice Tanzania, Ronald Shelukindo (katikati) akifafanua jambo wakati wa hafla mchapalo katika kusheherekea usiku wa Africa Day na DStv. Kulia ni Meneja Masoko wa Kampuni hiyo Furaha Samalu na kushoto ni Meneja Uhusiano wa Kampuni hiyo Barbara Kambogi.

Waalikwa katika hafla mchapalo ya kusheherekea usiku wa Africa Day na DStv katika Hoteli ya New Africa ya jijini Dar usiku wa kuamkia leo.

Kutoka kushoto ni Meneja Masoko wa Multichoice Tanzania Furaha Samalu, Blogger John Bukuku wa Fullshangwe Blog, Meneja Uendeshaji wa kampuni hiyo Ronald Shelukindo, Mdau wa DStv na Meneja wa Fedha katika kampuni hiyo Bw. Francis Senguji wakipozi kwa picha.
Meneja Uhusiano wa MultiChoice Tanzania, Barbara Kambogi (kulia) akifurahi jambo Wanahabari Sidi Mgumia (katikati) na Mama Mhina.
Ronald Shelukindo na Mdau LEMUTUZ wa Blog ya jamii.
Kutoka kushoto ni Meneja Masoko wa Multichoice Tanzania Furaha Samalu, Meneja Uendeshaji wa kampuni hiyo Ronald Shelukindo, Meneja wa Fedha katika kampuni hiyo Bw. Francis Senguji na mdau wa DStv wakipozi mbele ya camera yetu wakati wa hafla ya kusheherekea African Day na DStv iliyowakutanisha waandishi wahabari kutoka vyombo mbalimbali nchini.
Bloggers wakishow love…Kutoka kushoto ni Mkurugenzi wa Fullshangwe Blog John Bukuku, William Malecela wa Blog ya wananchi a.k.a LEMUTUZ na Operations Manager wa Mo Blog Zainul Mzige a.k.a Bigzee katika hafla mchapalo ya kusheherekea African Day na DStv katika Hoteli ya New Africa jijini Dar es Salaam.
Wanahabari wakiwa bize kujaza Quiz iliyotolewa na kampuni ya Multichoice Tanzania ambapo mshindi kwanza amezawadiwa Full Set ya King’amuzi cha Dstv na ‘Subscription’ ya mwezi mmoja na washindi kumi wamezawadiwa kofia na T-shirts za Supersport moja ya chaneli zinazopatikana katika king’amuzi cha Dstv.
Wanahabari wakiendelea kuumiza kichwa huku wengine waki-google majibu ya Quiz hiyo kupitia simu zao za kiganjani.
Mtangazaji wa Radio Dennis Buslwa a.k.a Ssebo (kulia) akiwa busy kutafuta majibu ambapo tunahisi alikwa anawasiliana na watu wa Mo Blog wampe majibu kamili. Wengine ni Kamera Man wa Channel Ten na Mtangazaji wa Radio Salma Msangi pamoja na mdau wa Star Tv.
Barbara Kambogi akiteta jambo na Angela Msangi wa TBC.
Dada Revina Bandihai wa kampuni ya Multichoice Tanzania na HR Manager wa kampuni hiyo.
Ronald Shelukindo na Dada Furaha Samalu wakifungua mziki wa Kiafrika huku Bw. Francis Senguji akiserebuka na mdau.

Mkurugenzi wa Fullshangwe Blog John Bukuku akiserebuka na Meneja Uhusiano wa Multichoice Tanzania Barbara Kambogi wakati wa hafla hiyo.

Salma Msangi akionekana Kiafrika zaidi akiyarudi na Khadija Kalili wa Jambo leo.

Kwaito ilichezeka kisawa sawa….Chezea Multichoice wewe…..Ilinogaje.!
Kutoka kushoto ni Blogger Cathbert Angelo wa kajunason Blog, Mpiganaji Fadhili Akida na Blogger Othman Michuzi wa mtaa kwa mtaa Blog wakipoowz mbele ya kamera yetu.
Bloggers katika picha ya pamoja.
Dada Revina Bandihai wa Multichoice Tanzania na Bw. Francis Senguji wakisataka Rhumba wakati wa hafla hiyo.
Meneja wa Fedha wa Multichoice Tanzanua Bw. Francis Senguji akimpongeza Ssebo baada ya kuibuka mshindi katika Quiz iliyoendesha na Kampuni hiyo ambapo alinyakua Full Set ya King’amuzi cha Dstv na ‘Subscription’ ya mwezi mmoja.

Pichani juu na chini Meneja Uhusiano wa Multichoice Tanzania Barbara Kambogi akigawa Kofia na T-shirts kwa washindi wa Quiz ilyoendeshwa na kampuni hiyo wakati wa kusheherekea Africa Day na Dstv.

Dada Revina Bandihai (kushoto) wa Multichoice Tanzania akishow love na washindi wa Quiz iliyoendeshwa na kampuni hiyo.
Wanahabari wakishow love…Thank you DStv for the Cocktail Party to celebrate Africa Day with DStv.

Kongamano la Wanafunzi kufanyika Musoma



CONGAMANO
 
TAASISI ya kuhamasisha maendeleo na mawasiliano katika jamii yenye makao yake mjini Musoma mkoani Mara ya JAMII INFORMATION NETWORK inatarajia kufanya Kongamano kubwa litakalo wahusisha  Wanafunzi zaidi ya 200 kutoka Shule 10 za Sekondari za Manispaa ya Musoma Mwezi Agosti mwaka huu, ikiwa ni njia ya kuhamasisha Maendeleo na uimarishaji wa Mawasiliano ndani ya Jamii.
Katika Kongamano hilo mada mbalimbali zitatolewa na Wataalamu waliobobea katika Masuala ya uhamasishaji wa Vijana Kupambana dhidi ya Ukimwi,ujasiriamali,dhana ya kujiajiri,Changamoto katika Elimu kwa Vijana  pamoja na Ukatili wa Kijinsia ikiwa ni njia ya kujenga msingi bora wa makuzi kwa vijana wetu.
Mbali na hivyo vijana hao pia wataelezwa jinsi ya kuwa Wazalendo katika nchi yao,kupambana na rushwa,Umaskini lakini pia wakipata elimu sahihi ya faida za uwekezaji kwa Tanzania,Sababu za Mimba za Mapema kwa watoto wa kike na jinsi ya kujenga Mahusiano na Mawasiliano yaliyo sahihi.
Pamoja na Mtandao huu kuwa na nia njema katika kuwasaidia vijana lakini bado kumekuwepo na changamoto mbalimbali katika kufanikisha Kongamano hilo hasa katika Suala la kifedha,hivyo basi Taasisi ya JAMII INFORMATION NETWORK kwa nia njema inakuomba wewe Mtanzania,mpenda maendeleo,unaekaa ndani au nje ya nchi,Mashirika kusaidia taasisi hii katika kufanikisha kongamano hilo ili vijana wetu wakue katika makuzi mema na kujenga Tanzania ya kesho  iliyostaarabika.
Chanzo:Full Shangwe

Matokeo ya Kidato cha Sita kuchelewa kutoa kisa...!



Naibu Waziri wa Elimu, Philipo Mulugo

MATOKEO ya mtihani wa kidato cha sita yaliyotarajiwa kutangazwa mwezi  huu yatachelewa  ili kutoa nafasi kwa Baraza la Mitihani la Taifa (Necta),  kurekebisha matokeo mabaya ya mitihani  kidato cha nne ya mwaka jana yaliyofutwa na serikali  mwezi huu.

Matokeo ya kidato cha sita ambayo huwa yanatangazwa mwanzoni  mwa mwezi Mei mpaka sasa hayajatolewa  na kwamba hayatatangazwa mpaka matokeo mapya ya kidato cha nne yatakaporekebishwa rasmi.
Alipoulizwa  juu ya suala hilo, Naibu Waziri   wa Elimu na  Mafunzo ya Ufundi  Philipo Mulugo alisema ingawa wakati huu ndio unaopaswa yatangazwe matokeo ya kidato cha sita haitafanyika hivyo hadi yatangazwe matokeo mapya ya kidato cha nne baada ya kufutwa.

Hata hivyo, akasema huenda yakatolewa  pamoja au yakafuata wakati mwingine lakini mara baada ya  kukamilisha kazi ya kurejea na kusahihisha matokeo ya kidato cha nne.

"Siyo kwamba yamechelewa kwani muda wa kujiunga na chuo ni Septemba hivyo haitawaathiri kwa hilo," alisema Mulugo.

Kuhusu hatma ya wanafunzi wa kidato cha nne ambao wapo mashuleni wanaendelea na masomo ya kidato cha sita, alisema  kama kutakuwa na wanafunzi ambao wapo madarasani  shule zilizowasajili  zitakuwa hazijafuata mfumo wa elimu unavyoelekeza.

Alifafanua kuwa mfumo wa elimu kwa kidato cha nne ulibadilishwa na kwamba endapo mwanafunzi akifaulu anatakiwa kujiunga rasmi kidato cha sita  Julai na si vinginevyo.

Alisema licha ya  ucheleweshaji  wa matokeo  hali hiyo haikuwaathiri wanafunzi hao kwa kuwa ratiba ya kwenda masomoni  haijaanza kwa mujibu wa kalenda  ya shule ya serikali.

Serikali ilifuta matokeo ya kidato cha nne ya 2012 na kuiagiza Necta kuyaandaa upya kwa kutumia utaratibu wa usahihishaji na upangaji madaraja uliotumiwa mwaka  2011

Taarifa ilisema mfumo uliotumika  mwaka jana na kusababisha wanafunzi kushindwa vibaya haukufanyiwa utafiti na maandalizi ya kutosha kabla ya kutumika.

Matokeo hayo  yaliyotangazwa  mwezi  Februari mwaka huu yalionyesha kuwa asilimia 60 ya wanafunzi walishindwa mtihani.

CHANZO NIPASHE

Wajasiliamali wanawake nchini 'wafundwa'


Afisa Masoko wa Benki ya CRDB, Emmanuel Kiondo akizungumza na wa jasiriamali wanawake (hawapo pichani) kwenye mkutano uliofanyika jana jijini dar es salaam, ambapo nami kama Mwanamakuka namba mbili na wezangu tulishiriki mwanzo mwisho, ambapo kuna mambo mengi tumejifunza na kututia moyo katika harakati zetu za kujikwamua kiuchumi Tanzania.
WAJASIRIAMALI wanawake nchini wametakiwa kutumia vema fursa zenye tija zilizopo katika Akaunti ya Malkia ya Benki ya CRDB ili kuharakisha harakati za maendeleo yao kibiashara na kijamii.

Hayo yalisemwa na Ofisa Masoko Benki ya CRDB, Emmanuel Kiondo akiwasilisha mada katika kongamano la wanawake lililofanyika jijini Dar es Salaam jana, kwenye ukumbi wa Golden Jubilee Tower likihusisha wajasiriamali wanawake.

Kiondo alisema kuwa harakati za maendeleo kwa mwanamke ni muhimu kwa ustawi wa taifa na jamii na Malkia ya CRDB, ni njia sahihi itakayomuwezesha mjasiriamali huyo kuokoa pato lake ambalo awali lilikabiliwa na changamoto nyingi.

“Malkia Akaunti ni mkombozi wa kweli wa mjasiriamali mwanamke, ikibeba tija nyingi na kumuepushia adha zilizopo katika aina nyingine ya uwekezaji. Akaunti hii inatoa mkopo wa dharura wakati wa matatizo, wa asilimia 80 ya akiba yako, bila kuathiri chochote,” alisema Kiondo.

Aliwakumbusha wanawake kuhakikisha wanaepuka kero na changamoto zinazohatarisha harakati zao, kwa kuwekeza pesa zao kupitia akaunti hiyo, ambayo imewanufaisha wengi miongoni mwa wanawake wenye malengo tofauti.

Kongamano hilo la wanawake lilifanyika chini ya udhamini wa CRDB kupitia akaunti ya Malkia.

Wakizungumzia kongamano hilo, baadhi ya washiriki walipongeza mada na ushuhuda uliotolewa na waelimishaji, ambao umewaongezea hamasa katika kukabiliana na changamoto mbalimbali za kibiashara na kupanua wigo wa maendeleo yao.

Washiriki mbali walipata fursa ya kujifunza namna wajasiriamali walivyoweza kuinuka kutoka chini mpaka kumudu kumiliki viwanda vidogovidogo na kuwatia moyo wengine wanaoinuka kwa sasa.
Kongamano hilo liliandaliwa kwa ushirikiano baina ya Vocacom,  na CRDB pamoja na Maji ya Umoja, Jarida la Bhang, A1 Outdoor na wengine.

Thursday, 9 May 2013

Wajasiriamali wanawake kukutana Dar Siku ya Mama


MWENYEKITI wa Umoja wa Wanawake (UWT) Ilala, Nora Mzeru, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya Siku ya Mama iliyoandaliwa na Miss Earth, Bahati Chando, yatakayofanyika Mei 12, mwaka huu.

Siku hiyo itakuwa maalumu kwa mama na itawajumuisha wanawake wajasiriamali pamoja na wanawake wengine ambapo itafanyika katika Hoteli ya Lamada ya jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Bahati alisema wanawake wajasiriamali wataungana na wengine katika kufurahia siku hiyo, kubadilishana mawazo na kujengeneana uwezo katika masuala mengine ya ujasiriamali.

“Lengo la kufanya sherehe hizi ni kutaka wanawake kuungana kwa pamoja na wanawake wenzao duniani ikiwa ni pamoja na kubadilishana uzoefu katika kazi mbalimbali hasa zile za ujasiriamali kwa kuwa wanawake wanaweza,” alisema Bahati.

Aliongeza kuwa madhumuni ya maadhimisho hayo ni kutambua umuhimu wa mama, ambapo kaulimbiu ya mwaka huu ni: ‘Mara zote katika mioyo yetu inaonesha jinsi mama alivyo katika mioyo ya wote.’

Watanzania wahimizwa matumizi ya teknolojia

Mheshimiwa Raymond Mbilinyi


WATANZANIA wamehimizwa kujiwekea mikakati juu ya matumizi ya sayansi na teknolojia katika sekta mbalimbali za uzalishaji ili nchi ipige hatua za kiuchumi na kuboresha ustawi wa jamii.
Rai hiyo imetolewa na Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Biashara (TNBC), Raymond Mbilinyi alipokuwa katika mkutano wa majadiliano ya ushirikiano wa manufaa ya wote (Smart Partinership Diologue) uliofanyika mjini Morogoro.
Mbilinyi Sayansi na Teknolojia ina nafasi kubwa ya kuleta maendeleo endelevu nchini hivyo watanzania waizingatie katika kuzitumia bila woga wala kusita.
Alisema hata Malaysia inayotamba kwa sasa kiuchumi imefika hapo ilipo kutokana na kuzingatia matumizi ya nyenzo hizo.
Mkutano huo ulifanyika kwa kushirikisha makundi ya wananchi kutoka mikoa ya Morogoro, Tanga na Pwani na ilihudhuriwa pia na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Joel Bendera ambaye alishukuru serikali kupitia TNBC kwa kuleta fursa ya wananchi kuzungumzia na kujadili kwa uwazi masuala mbalimbali ya kimaendeleo.

Wananchi Lindi wajitolea kumjengea nyumba mwalimu

Wakati mwingine vikao kama hivyo kati ya viongozi na wananchi husaidia kuamsha ari ya maendeleo ya maeneo husika.

WANANCHI wa kata ya Chiola Halmashauri ya Wilaya ya Nachingwea mkoani Lindi wamechanga kiasi cha Sh. Mil. 18.9 kwa ajili ya ujenzi wa nyymba wa Shule yao ya Sekondari ya kutwa.
Ofisa Mtendaji wa Kata hiyo, Patricia Mbunda alisema mradi huo wa nyumba hiyo ya mwalimu uliibuliwa na Kamati ya Maendeleo ya Kata yao pamoja na wananchi wa eneo hilo kwa nia ya kumuondolea kero mwalimu huyo na walimu wengine ambao pia wanatarajiwa kujengewa hapo baadaye.
Mbunda alisema mradi wao umekusudia kujenga nyumba saba za walimu ili kuwatatulia kero walimu wa shule hiyo na wazo hilo lilipowasilishwa kwa wananchi, wakazi hao walionyesha ushirikiano kwa kuchangia Sh  Mil.5.9 wakati serikali kuu imetoa Sh Mil 13.
Alisema mradi huo wa kuwajengea nyumba walimu wa shule ya kata yao ulianza rasmi katikati ya mwaka jana na anashukuru namna wakazi wa kata hiyo walivyoonyesha kujali na kuthamini maendeleo ya elimu katika eneo lao na kuwapongeza waendelee na moyo huo huo kwa manufaa ya kata yao na taifa kwa ujumla.
"Kwa sasa tuna nyumba moja tu ya walimu kati ya saba tulizopanga kuzijenga, ila tunashukuru wananchi walivyojitolea, japo kazi bado kabisa kwani walimu wengine sita wanaishi nyumba za kupanga ambazo hazina ubora unaendana na hadhi ya walimu," alisema.
Unadhani wananchi wa maeneo mengine wangeiga mfano huu wa Kata hii ya Chiola, walimu wetu si wangepumua na kujionea fahari taaluma yao! Tuzinduke tusaidiane.

Wednesday, 8 May 2013

Wanafunzi Umbwe wagoma kula

   
MGOGORO umeibuka katika Shule ya Sekondari Umbwe kati ya wanafunzi wa kidato cha tano na uongozi wa shule hiyo hali iliyosababisha baadhi ya wanafunzi kugoma kula na kufanya maandamano wakishinikiza kuonana na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro kwa lengo la kutatua kero zilizoko shuleni hapo.

Kutokana na mgogoro huo, Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Dk. Ibrahim Msengi aliyefika shuleni hapo kuutatua, alimtaka Ofisa Elimu Mkoa Kilimanjaro kupeleka wakaguzi katika shule mbalimbali za sekondari ikiwemo ya Umbwe ikiwa ni hatua mojawapo ya kubaini walimu wanavyotekeleza wajibu wao.

Akizungumza na uongozi wa shule hiyo pamoja na wanafunzi hao, Msengi alisema hatua ya ukaguzi katika shule za sekondari hasa za serikali, itabainisha uchafu uliojificha ambao unachangia kutofanya vizuri kwa shule hizo.

Dk. Msengi alisema licha ya madai ya wanafunzi hao kukiuka taratibu za kufikisha madai yao, bado yana msingi kutokana na ukweli kwamba wanalalamikia kutofundishwa baadhi ya masomo, jambo ambalo alieleza ndiyo chanzo cha kufeli kwa wanafunzi.

“Mengi ya madai haya yangeweza kutatuliwa hapa shuleni tena bila hata kumuita mtu yeyote,” alisema Msengi huku akiwaomba wanafunzi kuwa na subira wakati suala hilo likipatiwa ufumbuzi.

Dk. Msengi aliwataka wanafunzi kurudi darasani kuendelea na vipindi kama kawaida wakati wakisubiri utatuzi wa malalamiko yao.

Katika hatua nyingine mkuu huyo wa wilaya alimtaka mkuu wa shule hiyo, Silvanus Lyome kufuatilia kwa karibu utendaji kazi wa walimu wanaolalamikiwa kuhakikisha lugha zisizoeleweka hazitumiki katika malezi ya wanafunzi hao.

Chanzo:Tanzania Daima

Mvua yasababisha upungufu wa madawati

   
WANAFUNZI 193 wanaosoma Shule ya Msingi Madaraka, Kata ya Mkwatani, wilayani Kilosa, Morogoro wanakaa chini kutokana na upungufu wa madawati.

Mwalimu Mkuu Msaidizi wa shule hiyo, Julieth Kalumwa, alisema jana kuwa wanafunzi wanaosoma darasa la awali na la kwanza wote wanakaa chini, na kwamba hiyo imechangiwa na madawati kuharibiwa vibaya na maji ya mafuriko.

Aliongeza kuwa wanafunzi wa darasa la pili na la saba pekee wanakaa kwenye madawati na kwamba madarasa yaliyosalia yana upungufu wa madawati na baadhi ya wanafunzi wanakaa chini.

Aidha, alisema shule hiyo kabla ya kukumbwa na mafuriko ilikuwa haina upungufu wa madawati, na kwamba yaliyokuwepo yalinyonya maji na hivyo kuharibika.

Mbali na hilo, alisema wanakabiliwa na uhaba wa vitabu vya kujifunzia na kufundishia, ambapo vya awali viliharibiwa na mafuriko, hivyo kupata wakati mgumu katika ufundishaji.

Kaimu Ofisa Elimu ya Msingi Wilaya ya Kilosa, Theodulis Mangia, alipoulizwa juu ya uhaba wa madawati alisema hilo ni la tatizo la wilaya nzima, huku akisema wanasubiri mgawo kutoka Tamisemi, ili kupunguza tatizo hilo.

HakiElimu yapinga kufutwa kwa matokeo ya mitihani ya Kidato cha 4

   


SERIKALI imetakiwa kuacha kukurupuka kufuta matokeo ya kidato cha nne mwaka 2012 kutokana na sababu za msingi za kufeli kwa wanafunzi hao zinafahamika.

Hayo yalielezwa jana jijini Dar es Salaam na muungano wa asasi tano za kiraia uliowakilishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa HakiElimu, Elizabeth Missokia.

Asasi zilizotoa tamko la pamoja huku zikipendekeza njia sahihi ya serikali kuwekeza katika elimu ni pamoja na Hakielimu yenyewe, Policy forum, Sikika, TenMet na TGNP.

Kwa niaba ya mitandao hiyo mkurugenzi huyo alisema hakukuwa na haja ya kufuta matokeo hayo na kufanya maboresho kwa kuwa sababu zilizosababisha kufeli kwa wanafunzi zinajulikana na si kama serikali inavyodai kwa sasa.

Missokia alisema kabla ya serikali kutoa uamuzi huo ilitakiwa kuweka wazi mapendekezo ya Tume ya Waziri Mkuu iliyoundwa kuchunguza matokeo hayo ili wadau wa elimu wapate fursa ya kuona sababu zilizochangia kushuka kwa ufaulu katika mitihani hiyo.

“Kwa kufuta matokeo hayo bila wadau kujua sababu na kutoa mchango wao inawaaminisha Watanzania kwamba sababu nyingine hata kama zipo ziliathiri kwa kiwango kidogo matokeo hayo na suala la upangaji wa madaraja kuonekana ni sababu kubwa zaidi kuliko nyingine,” alisema Missokia.

Alisema hiyo sio sababu kwani matokeo ya kidato cha nne yaliyopita huku akiyataja ya mwaka 2009 yalikuwa asilimia 27.5 ya watahiniwa waliopata daraja sifuri, mwaka 2010 sifuri walikuwa 49.6 na mwaka 2011 asilimia 46.4 ambayo ni matokeo mabaya pia.

Alisema kwa mtiririko huo wa matokeo ni lazima kulikuwa na sababu kubwa zaidi iliyochangia kushuka kwa ufaulu na kwamba hakuna uhusiano wa moja kwa moja kati ya kubadili utaratibu wa kupanga matokeo na ufaulu duni wa 2012.

Ilielezwa kuwa sababu nyingine ni kutokuwa na walimu wa kutosha hasa kwa masomo ya sayansi; shule kuwa na upungufu mkubwa wa vitabu na vifaa mbalimbali vya kujifunzia na kufundishia; bajeti ya maendeleo shuleni kuwa ndogo; ruzuku mashuleni kufika ikiwa pungufu na wakati mwingine ikiwa imechelewa; mihtasari ya kufundishia ina mkanganyiko mkubwa; na huku mtaala mpya wa mwaka 2005 ukiwa mgeni kwa walimu walio wengi.

“Msingi mbovu wa lugha ya Kiingereza ambayo ndiyo lugha ya mawasiliano darasani; walimu kutokuwa na hamasa ya kufundisha kutokana na madai ya muda mrefu na kufanya kazi katika mazingira magumu sambamba na kukosekana kwa mafunzo kazini ya kuwaimarisha katika ufundishaji wao; na hamasa ndogo miongoni mwa wazazi katika kufuatilia malezi ya watoto wao,” alisema Missokia.

Hata hivyo alieleza kuwa kuandaliwa upya kwa matokeo hayo, serikali inatakiwa ikumbuke kuna athari mbalimbali ambazo zitatokea ikiwa ni pamoja na baadhi ya wanafunzi ambao walijiua baada ya kupata matokeo mabaya.

“Sasa endapo watapata alama za juu nani atakayetakiwa kuwajibishwa kwa hilo?”

Pia kuna baadhi ya wanafunzi na wazazi wameshafanya maamuzi mbalimbali, pamoja na waliokata tamaa na wamepata madhara makubwa kisaikolojia na wengine kukubali kurudia mitihani na kuhoji serikali itatoa fidia gani.

Pia waliwashukia NECTA kutokana na kukanusha kutumika kwa utaratibu mpya wa upangaji wa madaraja huku wakihoji hivyo iliwadanganya Watanzania.

Asasi hizo pia zilieleza kuwa kwa kuwa serikali imeamua kufuta matokeo hayo na hatimaye kupangwa upya kwa utaratibu wa mwaka 2011 zilishauri zoezi hilo kufanyika kwa uwazi kwa kushirikisha wadau wengine wa elimu ili kujiridhisha na uhalali wa alama za wanafunzi zitakazokuwa zinarekebishwa na siyo uchakachuaji katika njia za urekebishaji na upangaji wa matokeo katika madaraja.